IQNA

Sheikh Sabri aonya kuhusu kushadidi njama za Israel dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa

18:51 - May 03, 2025
Habari ID: 3480627
IQNA-Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) ameonya kuhusiana na kushadidi mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya msikiti huo na mji wa Quds, na hivyo ametoa mwito wa kukabiliana mara moja na vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu vinavyosimamiwa na utawala haramu wa Israel.

Sheikh Ekrima Sabri  amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel umepanua wigo wa uvamizi wake dhidi ya Masjdul Aqsa tangu kulipianza vita vya Gaza.

Sheikh Sabri amebainisha kwamba, wavamizi wanatekeleza siasa za kuwabaidisha kwa umati Wapalestina jambo ambalo halifanyika sehemu yoyote ile duniani.

Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.

Walowezi wengi wa Kizayuni wenye misimamo mikali mara kwa mara wamekuwa wakivamia msikiti wa al-Aqsa kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel.

Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqsa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Israel ilikalia kwa mabavu Mashariki ya al-Quds, ambapo Al Aqsa inapatikana, wakati wa Vita vya Waarabu na Israel vya 1967. Israel iliuteka mji wote wa Quds 1980 kwa hatua ambayo haikuwahi kutambuliwa na jamii ya kimataifa. Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilitangaza mnamo Julai 2024 kwamba ukaliaji wa muda mrefu wa Israel wa maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria, na kuhitaji kuhamishwa kwa makazi yote katika Ukingo wa Magharibi na Mashariki ya al-Quds.

/3492914

Habari zinazohusiana
Kishikizo: Ekrima Sabri al aqsa
captcha