IQNA

Kadhia ya Palestina

Sauti ya Adhana kusikika Palestina milele

20:47 - December 03, 2024
Habari ID: 3479850
IQNA – Sheikh Ekrema Sabri, Imamu wa Msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel, amesema sauti ya Adhana (wito wa Waislamu wa kuswali) itaendelea kusikika huko Palestina milele.

"Sauti ya Adhana imesikika katika anga ya Palestina tangu wakati wa Bilal al-Habashi, muadhini wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW), na itaendelea kuwa hivyo hadi Siku ya Kiyama," Sheikh Sabri alisema.

"Mtu yeyote ambaye anatatizwa na wito wa kuswali anaweza kuondoka," ameongeza.

Ameyasema hayo akijibu matamshi ya waziri mwenye misimamo mikali ya kufurutu ada wa utawala ghasibu wa Israel Itamar Ben-Gvir ambaye ametoa wito wa kuondolewa vipaza sauti kutoka misikiti ya miji ya Kiarabu ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Ben-Gvir, mwanasiasa mwenye utata wa mrengo mkali wa kulia, amevitaja vipaza sauti kama "chanzo cha fujo" katika taarifa ya umma siku ya Jumamosi.

Sheikh Sabri amesema Adhana ni ibada ya Kiislamu inayofungamana na Swalah ambayo ni kitendo cha faradhi katika Uislamu, na hakuna anayeweza kuizuia.

Amesisitiza kuwa kuzuia Adhana ni kuingilia masuala ya kidini ya Waislamu na ukiukaji wa uhuru wa kidini na haki zinazodhaminiwa na sheria za kimataifa.

Matamshi ya Ben-Gvir yameleta lawama nyingi. Baraza la Kitaifa la Palestina, chombo cha juu zaidi cha maamuzi kwa Wapalestina, kilitoa taarifa siku ya Jumapili kulaani matamshi hayo na kuyataka kuwa ni "uhalifu" dhidi ya maeneo ya ibada.

Baraza hilo lilitaja hatua hiyo kuwa “shambulio la waziwazi kwenye maeneo matakatifu na desturi za kidini,” likisisitiza kwamba haki hizo zinalindwa chini ya sheria za kimataifa na za kibinadamu.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas , pia ililaani kauli ya Ben-Gvir, na kuuita "uhalifu mkubwa na shambulio dhidi ya uhuru wa kuabudu".

Katika taarifa, kundi hilo limewataka Wapalestina kupinga uamuzi huo na kupinga majaribio ya kudhoofisha desturi zao za kidini na maeneo matakatifu.

Hamas ilitoa wito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, na mashirika ya kimataifa kukemea tamko hilo, kuishinikiza Israel kusitisha vitendo hivyo, na kuwawajibisha watawala wa Israel  kwa ukiukaji wa haki za Wapalestina na maeneo matakatifu.

3490919

captcha