Ayatullah Abbas Kaabi alibainisha tathmini yake kuhusu matukio yanayoendelea nchini Syria katika makala ambayo ameiandika katika Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA).
Vikosi vya upinzani vyenye silaha, vikiongozwa na Hay’at Tahrir al-Sham (HTS), viliingia mji mkuu Damascus siku ya Jumapili, siku chache tu baada ya kuanzisha mashambulizi huko Aleppo (Halab). Hii iliashiria mwisho wa zaidi ya miongo mitano ya utawala wa ukoo wa Assad nchini Syria.
"Madhara ya tukio hili yatakuwa makubwa kikanda na kimataifa," Ayatullah Kaabi alisema, akitaja uvamizi wa Israel katika maeneo ya kusini mwa Syria kama moja ya matokeo ya awali ya kuangushwa serkali ya Assad.
Aliendelea kutaja sababu nne za kuanguka kwa serikali ya Syria. Mwanazuoni huyo kwanza ametaja "mmomonyoko katika muundo wa serikali na jeshi la Syria, pamoja na uchovu na ukosefu wa motisha."
"Azma dhaifu na kutokuwepo kwa mpango wa uendeshaji wa kukabiliana na vikosi vya upinzani vyenye silaha," na "Uzembe wa kimkakati na sambamba na kuhadaiwa na Marekani na washirika wake wa kikanda, kuweka kipaumbele kwa maelewano na mazungumzo (na maadui wa zamani) badala ya kutegemea kambi ya muqawama (Iran, Hizbullah, Ansarullah, Hamas, Kataib Hizbullah, Jihad Islami na harakati zinginezo) " zilikuwa sababu nyingine mbili zilizotajwa na Ayatullah Kaabi.
Vile vile amebainisha kuwa serikali ya Syria ilishindwa kuzingatia maonyo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kwamba madola ya Magharibi na waitifaki wao wa kieneo yanakusudia kuuangusha mfumo wa kisiasa wa Syria kwa njia zisizokuwa za vita na hivyo kuiondoa nchi hiyo katika duara la madola yenye satwa kieneo.
"Ahadi tupu za Magharibi"
"Kushindwa huku kwa serikali ya Bashar al-Assad kunatokana na kuegemea vibaya kwa ahadi tupu za nchi za Magharibi na waitifaki wao wa kikanda," alisisitiza.
Ayatullah Kaabi alimnukuu marehemu kiongozi wa Hizbullah ya Lebanon Seyyed Hassan Nasrallah, akibainisha kuwa Syria ilitoa uungaji mkono kwa Lebanon katika vita vya mwaka 2006, ambavyo hatimaye vilipelekea kushindwa kwa utawala wa Israel.
"Kwa bahati mbaya, kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa (ya Okotoba 7 2023 ya Hamas dhidi ya Israel), serikali iliyochakaa ya Syria na jeshi lake ilisalimu amri mbele ya vitisho, vishawishi, na vita vya kisaikolojia, wakichagua maelewano na maadui badala ya kuegemea kambi ya Muqawama. Ikiwa wangechagua njia ya Muqawama, hawangeshindwa,” alisema.
"Hasara hii isichukuliwe kimakosa kama kushindwa kwa harakati ya muqawama au Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," mwanazuoni huyo alisema, akibainisha kuwa Muqawama umeingia ndani kabisa ya mioyo ya mataifa na kwamba kuanguka kwa serikali ya Syria kunaweza kugeuzwa kuwa fursa ya kuimarisaha muqawama.
"Kwa bahati mbaya, hisia dhidi ya Iran na Waislamu wa madhehebu ya Shia, kuwepo kwa makundi yenye misimamo mikali miongoni mwa wapinzani, na njama za maadui dhidi ya kambi ya muqawama na Iran kumezua sintofahamu kali. Hata hivyo, kwa njia ya mazungumzo ya kina, ya wazi na ya kimkakati na wafuasi wenye busara wa upinzani miongoni mwa watawala wapya wa Syria, na kwa upatanishi wa makundi kama vile Hamas, Ikhwanul Muslimin, na baadhi ya nchi za kieneo, mfumo mpya unaweza kupendekezwa ili kuhakikisha maslahi ya kudumu ya watu wa Syria, Muqawama wa Kiislamu, na usalama wa kikanda, aliongeza.
Aliwaonya wale walio madarakani nchini Syria kuchukua somo kutokana na kuanguka kwa serikali ya Mohammad Morsi nchini Misri, akibainisha kwamba aliweka imani katika "ahadi potofu na tupu za Marekani na Magharibi."
"Wale walio madarakani sasa katika ukweli mpya wa Syria lazima walichukulie onyo hili kwa uzito: usiamini kamwe Marekani, Magharibi, au Wazayuni. Hakuna ahadi yoyote kati ya hizo itakayotimizwa, na kupuuza ushauri huu kunaweza kusababisha kuibuka mapinduzi mapya yanayoungwa mkono na Marekani au hata kugawanyika kwa Syria.”
Ayatullah Kaabi alibainisha kuwa ni muhimu kuzingatia mambo ya Waislamu, kustawisha umoja wa jumuiya ya Kiislamu, kuepuka misimamo mikali ya kidini na ukufurishaji, na kutatua hali ya kutoelewana ili kufungua sura mpya ya ushirikiano wa Kiislamu kupitia ujenzi wa muungano.
"Jamhuri ya Kiislamu mara kwa mara imekuwa ikikaribisha mpango au utaratibu wowote unaohimiza usalama, utulivu, maendeleo, uadilifu, utu na maslahi ya Umma wa Kiislamu," alisema na kusisitiza, "Umoja wa Kiislamu ni mkakati wa kuleta uhai na sio sera ya kupita.”
Mwanazuoni huyo ameashiria pia ulazima wa kuwepo muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni, uungaji mkono wa pande zote kwa watu wa Palestina na Ghaza, juhudi za pamoja za kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na kutetea haki za binadamu.
3491001