Kwa mujibu wa Idara Kuu ya Habari na masuala ya Usemaji ya Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa kuhusiana na matukio ya hivi karibuni ya Syria ambapo huku ikikumbusha msimamo wa kimsingi wa Iran wa kuheshimu umoja, mamlaka ya kitaifa na utimilifu wa ardhi Syria, imeeleza kuwa, kufikiwa jambo hili kunahitaji kuhitimishwa haraka mapigano ya kijeshi, kuzuia vitendo vya kigaidi na kuanza kwa mazungumzo ya kitaifa kwa kushirikishwa matabaka yote ya jamii ya Syria ili kuunda serikali jumuishi ambayo itakuwa na wakilishi wa watu wote wa Syria.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono taratibu za kimataifa zinazoegemezwa kwenye Azimio nambari 2254 la Umoja wa Mataifa la kufuata mchakato wa kisiasa nchini Syria kama ilivyokuwa hapo awali na inaendelea kushirikiana kiujenzi na Umoja wa Mataifa katika suala hili.
Iran imesisitiza kuhusu hadhi ya Syria kama nchi "muhimu na yenye ushawishi" katika eneo la Magharibi mwa Asia na haitaacha juhudi yoyote kusaidia nchi hiyo kuimarisha usalama na utulivu.
Kulingana na taarifa hiyo, Iran itaendelea na mashauriano yake na pande zote zenye ushawishi, hasa zile za eneo la Asia Magharibi.
"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuatilia kwa karibu matukio nchini Syria na katika eneo na itachukua hatua na msimamo unaofaa huku ikizingatia muelekeo wa wenye ushawishi katika uga kisiasa na usalama nchini Syria," imebaini taarifa hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imsisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa raia wote wa Syria na raia wa nchi nyingine pamoja na kuhifadhi utakatifu wa maeneo ya kidini na matakatifu.
Pia taarifa hiyo imesisitiza ulazima wa kulinda majengo ya kidiplomasia kulingana na sheria za kimataifa.
Halikadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeashiria uhusiano wa kina na wa kirafiki kati ya watu wa Iran na Syria na kusema: "inatarajiwa kwamba nchi hizi mbili zitaendeleza mbinu ya busara na yenye mtazamo wa mbali ili kudumisha uhusiano wa pamoja kulingana na maslahi ya kawaida."
4252998