Katika azimio la usitishaji vita huko Gaza, Baraza Kuu la UN limetaka vita hivyo visimamishwe mara moja, bila masharti, kwa kudumu na kuheshimiwa na pande zote, na kusisitizia pia kuachiliwa huru mara moja mateka wote na bila masharti yoyote.
Aidha, azimio hilo limetaka ufanyike ufikiaji wa haraka wa raia katika Ukanda wa Gaza kwa huduma za kimsingi na usaidizi muhimu wa kibinadamu kwa maisha yao, sambamba na kupinga hatua zozote za kuwasababishia njaa Wapalestina wa eneo hilo.
Kufanyika kwa kikao hicho cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kumechochewa na hatua ya Marekani kutumia kura ya turufu katika Baraza la Usalama na kukwamisha kusudio la kutekelezwa usitisha mapigano huko Ghaza, ambako kwa miezi 14 sasa utawala wa Kizayuni unaendesha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo uliloliwekea mzingiro.
Azimio hilo la usitishaji vita limepitishwa kwa wingi mkubwa wa kura 158 za 'ndiyo' kati ya kura 193 za wanachama wote wa Baraza Kuu, huku likipingwa na nchi tisa tu pamoja na nyingine 13 zilizoamua kutopiga kura.
Kama ilivyo kawaida, utawala wa Kizayuni wa Israel na muungaji mkono wake mkuu Marekani zilikuwa kwenye kundi la nchi chache zilizopiga kura za kupinga azimio hilo, ambalo halina ulazima wa kisheria wa utekelezaji.
Kwa upande wa azimio la pili kuhusu UNRWA, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limelaani sheria iliyopitishwa na Bunge la Israel (Knesset) tarehe 28 Oktoba 2024, ambayo imelipiga marufuku shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa Palestina kufanya kazi ndani ya maeneo yaitwayo Israel pamoja na Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi.
Vilevile limetoa wito kwa serikali ya Israel kutimiza wajibu wake wa kimataifa, kuheshimu haki na kinga za shirika hilo na kutekeleza wajibu wake wa kuruhusu na kuwezesha usaidizi kamili wa kibinadamu wa haraka, salama na usiozuiliwa katika aina zake zote ndani na katika Ukanda wote wa Gaza, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za kimsingi zinazohitajiwa sana na raia.
Azimio hilo limepitishwa kwa kura 159 zilizounga mkono, tisa zilizopinga; na nchi 11 ziliamua kutopiga kura.
4253767