IQNA

Muqawama

Oktoba 7; Siku Iliyobadilisha milingano ya kikanda

20:39 - October 07, 2024
Habari ID: 3479555
IQNA - Utawala wa Israel haujapata mafanikio yoyote yanayoonekana huko Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana zaidi ya kuwaua Wapalestina wapatao 42,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Uchambuzi wa medani ya vita katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa unaonyesha kuwa licha ya uharibifu mkubwa, Gaza sasa imekuwa sehemu muhimu katika mapambano ya miongo saba ya mataifa ya Kiislamu dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Katika historia, kumekuwa na mataifa ambayo yamepigana kwa miongo kadhaa dhidi ya wakoloni, waporaji, na wavamizi wa kigeni kwa ajili ya uhuru na utu wao na hatimaye kuibuka washindi.

Mifano ni pamoja na taifa la Iran wakati wa vita vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Algeria katika mapambano yake dhidi ya wakoloni wa Ufaransa, na Vietnam dhidi ya uvamizi wa Marekani. Mataifa haya yalilipa gharama kubwa lakini hayakujisalimisha. Hivi sasa Gaza iko katika hali kama hiyo, na ushindi wa watu wake bila shaka utakuwa na nafasi muhimu katika kubadilisha mienendo ya kieneo na kuchangia kusambaratika utawala huo dhalimu.

Mzingiro wa Gaza, uharibifu wa miundombinu yake, na kuwatimua wakazi wake kwa lazima na utawala wa Israel, kwa bahati mbaya, ulifanyika katika hali ya kimya cha jumuiya ya kimataifa na nchi za Kiarabu za eneo hilo.

Licha ya mashinikizo ya kieneo na kimataifa, Mhimili wa Muqawama (mapambano ya Kiislamu) ukiwa ndio muungaji mkono pekee wa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, umeisaidia Gaza kwa raslimali zake zote katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa jeshi la Israel. Kwa uhalisia, Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ilivuruga mikakati na matukio mengi yaliyowekwa ili kuangamiza muqawama na kutekeleza kile kinachoitwa Makubaliano ya Abraham.

Lau mpango huu ungetekelezwa katika eneo hili, suala la Palestina na muqawama wa Kiislamu lingewekwa kando kabisa, na utawala huo wa Kizayuni ungepata udhibiti wa hatima ya mataifa ya Kiislamu. Hii ingemaanisha kutekelezwa kwa mkakati wa Shimon Peres, waziri mkuu wa zamani wa Israel, kwa "Mashariki ya Kati Mpya " chini ya uongozi wa Israel.

Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ilifichua hali halisi ya baadhi ya tawala za Kiarabu zinazofanya mapatano na utawala haramu Israel na sasa tawala hizo zinazorota taratibu. Kama vile vita vya siku 33 vya Hizbullah na Israel, ambavyo viliishia kwa ushindi kwa muqawama wa Kiislamu, viliongeza umaarufu wa mhimili wa muqawam miongoni mwa watu wanaopenda uhuru duniani kote.

Ripoti zinaonyesha kuwa Israel imepata hasara na maafa makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, hasara isiyo na kifani katika historia yake ya miaka 76. Katika mwaka mmoja wa vita vya Gaza, idadi wanajeshi wa Israel waliouawa na kuelekea jahanamu ni  2,000 na 9,000 wamejeruhiwa, na wengine 15,000 wametoroka jeshini, pamoja na uharibifu wa mamia ya vifaru na hasara ya kifedha ya dola bilioni 100 wakati wa vita vya Gaza.

Uchokozi dhidi ya Iran

Katika kujaribu kuuepuka mzozo wa Gaza na kubadilisha mienendo ya mzozo huo, utawala wa Kizayuni uliamua kuchukua hatua za uchochezi dhidi ya Iran na mhimili wa muqawama. Hii ilijumuisha mauaji ya watu wenye ushawishi mkubwa kama vile Ismail Haniya, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, na Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah, kwa lengo la kuhamisha mgogoro wa Gaza nje ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Hata hivyo, jibu madhubuti la Jamhuri ya Kiislamu katika oparesheni mbili, Ahadi ya Kweli ya I na II, ulidhihirisha kuwa Iran ina uwezo mkubwa wa kumzuia adui, na hivyo kubainisha wazi kwamba hakuna mgogoro unaoweza kutatuliwa bila ya kwanza kupita kwenye milango ya Tehran.

Sasa, kutokana na kushindwa kijeshi na kisiasa, utawala huo ghasibu wa Israel umeamua kuanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya watu wa kusini mwa Lebanon ili kujaribu kupata ushindi wa haraka wa kijeshi. Hata hivyo, mashambulizi ya mabomu ya raia wasio na ulinzi huko Lebanon na Gaza hayataleta mafanikio ya kijeshi kwa Benjamin Netanyahu; badala yake, itaongeza tu wimbi la kimataifa la chuki dhidi ya utawala huo.

Ujumbe wa Swala ya Ijumaa Tehran

Swala ya Ijumaa ya hivi karibuni hapa Tehran iliyoongozwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei iliyohudhuriwa na viongozi wote wa Iran na mamilioni ya watu ilitoa ujumbe wa wazi kwa walimwengu.

Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake amesisitiza kuwa, iwapo utawala wa Israel utathubutu kuchukua hatua yoyote dhidi ya Iran, basi utakabiliwa na jibu kubwa zaidi. Mahudhurio makubwa ya wananchi wa Iran katika swala na khutba yenye nguvu iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu kwa lugha ya Kiajemi na Kiarabu ilidhihirisha nguvu za kitaifa na Kiislamu za Iran kwa walimwengu.

Kutokana na hali hiyo, mwaka mmoja baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, licha ya ukimya wa jumuiya ya kimataifa na tawala za Kiarabu ambazo zina Matano ya uhusiano na Israe, eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) linasimama kwenye ukingo wa mabadiliko ya kihistoria.

Mhimili wa Muqawama, licha ya mauaji ya shakhsia wenye ushawishi kama Sayyed Hassan Nasrallah, utaendelea na makabiliano yake na utawala wa Israel kwa usahihi wa kimbinu. Siku za mbele bila shaka zitakuwa zenye changamoto; iwapo utawala huo utaendelea na chokochoko zake, mhimili wa muqawam utajibu kwa nguvu kubwa zaidi sambamba na kuwepo mikakati mipya, na hatimaye kutengeneza njia ya kuanguka kwa utawala ghasibu wa Israel.

 Makala hii imeandikwa kwa lugha ya Kiajemi na Hassan Hanizadeh, mtaalamu wa Kiirani wa masuala ya kikanda, iliyochapishwa kwenye gazeti la Jam-e Jam mnamo Oktoba 7, 2024.

3490171

Habari zinazohusiana
captcha