IQNA

Jinai za Israel Gaza

Wataalamu wa UN waonya kuhusu mauaji ya kimbari Gaza, waliouawa wafika 11,500

21:46 - November 17, 2023
Habari ID: 3477903
TEHRAN (IQNA)- Wataalam wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kuzuia mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina wa Gaza huku utawala katili wa Israel ukiendeleza vita vyake dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.

Katika tarifa yao iliyotolewa mjini Geneva Uswisi Alhamisi, wamesema “Ukiukwaji mkubwa unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina baada ya shambulio la Oktoba 7, hususan Gaza unaelekea kuwa mauaji ya kimbari.

Wataalamu hao wameonyesha ushahidi wa kuongezeka uchochezi wa mauaji ya kimbari ambapo wameashiria nia ya wazi ya kuwaangamiza watu wa Palestina ambao ardhi yao inakaliwa kwa mabavu na Israel, wito mkubwa wa Nakba ya pili huko Gaza na eneo lote la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, na matumizi ya silaha zenye nguvu ambazo zimesababisha idadi kubwa ya vifo na uharibifu wa miundombinu muhimu katika maisha ya mwanadamu.

Wataalamu hao wamesema:  "Wengi wetu tayari tumetoa tahadhari kuhusu hatari ya mauaji ya kimbari huko Gaza."

Aidha wamebaini kuwa: "Tumesikitishwa sana na kushindwa kwa utawala wa Israel kutii wito wetu na kufikia usitishaji mapigano mara moja. Pia tuna wasiwasi mkubwa kuhusu namna baadhi ya serikali zinavyounga mkono mkakati wa vita wa Israel dhidi ya wakazi waliozingirwa wa Gaza, na kushindwa kwa mfumo wa kimataifa kuhamasishana kuzuia mauaji ya kimbari."

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wanasema vita vya sasa vya Gaza vinatokea wakati Israel inazidisha mzingiro wake usio halali wa miaka 16 dhidi ya Gaza, ambao umewazuia watu kukimbia na kuwaacha bila chakula, maji, dawa na mafuta kwa wiki kadhaa sasa." Wamesema vitendo hivyo vya Israel vya kusababisha njaa kwa makusudi ni sawa na uhalifu wa kivita.

Hali kadhalika wataalamu hao wamebainisha kuwa nusu ya miundombinu ya kiraia katika Ukanda wa Gaza imeharibiwa, ikiwa ni pamoja na zaidi ya nyumba 40,000 za makazi, pamoja na hospitali, shule, misikiti, mabekeri ya mikate, mabomba ya maji, maji taka na mitandao ya umeme, kwa njia ambayo imepelekea muendelezo wa maisha ya kawaida kwa Wapalestina huko Gaza kuwa jambo lisilowezekana.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wanasema Israel inasalia kuwa mamlaka inayokalia kwa mabavu ardhi za Palestina, ambayo pia inajumuisha Ukanda wa Gaza, na hivyo haipaswi kuanzisha vita dhidi ya wakazi ambao imekalia ardhi zao kwa mabavu.

Israel ilianzisha vita dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba baada Hamas kuendesha operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya Isreal ikiwa ni katika kukabiliana na jinai za Israel za miongo kadhaa za  umwagaji damu na uharibifu dhidi ya Wapalestina.

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, Israel imewaua Wapalestina wasiopungua 11,500, wakiwemo watoto 4,630 na wanawake 3,130, na kujeruhi wengine zaidi ya 32,000.

Hospitali zimekuwa kitovu cha mashambulio makali ya utawala dhalimu wa Israel tangu kuanza vita.

 

/4182175

Habari zinazohusiana
captcha