IQNA

Jinai za Isarel

MSF yaonya kuhusu hatua ambazo utawala wa Israel unachukua dhidi ya eneo la Rafah

16:00 - May 09, 2024
Habari ID: 3478796
Mkuu wa timu ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ametahadharisha kuwa mazingira ya kuidhaminia Gaza maji safi, chakula na dawa za matibabu yamefika marhala hatari na kwamba hatua ya kukifunga kivuko cha Rafah kunaifanya hali ya wakazi wa ukanda huo kuwa mbaya zaidi.

Aurélie Godard Mkuu wa timu ya Madaktari Wasio na Mipaka huko Gaza ametaka kufunguliwa kivuko cha Rafah na kusema misaada ya kibinadamu, vifaa tiba, chakula na fueli haviwezi tena kuingizwa Ukanda wa Gaza. 

Godard ametahadharisha kuhusu kupungua pakubwa huko Gaza maji safi, chakula na dawa za matibabu na kuongeza kuwa: Baada ya kupita miezi saba ya vita ambavyo vimesababisha watu milioni moja na laki saba kuhama makazi yao; uamuzi wa kukifunga kivuko cha Rafah utazidisha tu hali mbaya kwa wakazi wa Gaza. 

Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametahadharisha kuwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika mji wa Rafah yatasababisha maafa ya binadamu na kuyataja kuwa ni kosa la kistratejia. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameutaka utawala wa Kizayuni na harakati ya Hamas kufikia makubaliano ya usitishaji vita na kuzuia uvamizi kamili wa utawala huo mjini Rafah.

Uamuzi wa Israel wa kushambulia Rafah 

Siku ya Jumatatu (tarehe 6 Mei), baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni wa Israel liliidhinisha shambulio la ardhini dhidi ya mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza licha ya upinzani wa kimataifa. Jeshi la utawala wa Israel limekalia kwa mabavu sehemu ya kivuko cha Rafah mashariki mwa mji huo tangu juzi Jumanne.

Katika hali ambayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kukubaliana na mpango wa usitishaji vita wa Misri na Qatar, utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha mashambulizi makali dhidi ya mji wa Rafah huko Ukanda wa Gaza.

Zaidi ya miezi 7 sasa imepita tangu Israel ianzishe vita na mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Gaza. 

Inaonekana kuwa, sisitizo la utawala wa Kizayuni la kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Rafah na wakazi wake linatokana na mambo matatu.

Kwanza ni kwamba, baraza la mawaziri la Netanyahu linaundwa na watu wenye hitilafu na tofauti za kifikra, kitabia na kitaaluma. Kwa sababu hii tunaona kuwa, wakati baadhi ya wajumbe wa baraza la mawaziri la Netanyahu wakisisitiza ulazima wa kusitishwa mapigano, watu wengine kama vile Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala haramu wa Israel, wanatishia kuondoka kwenye baraza la mawaziri iwapo jeshi halitaushambulia mji wa Rafah.

Pili ni kuwa, Benjamini Netanyahu anaona kuwa anapaswa kuendeleza vita ili aendelee kuweko madarakani. Kuhusiana na jambo hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman al-Safadi, amekosoa uamuzi wa utawala wa Israel wa kuishambulia Rafah na kusema kuwa, Netanyahu anataka kupanua vita ili kulinda mustakabali wake wa kisiasa.

Jambo la tatu ni kuwa, utawala wa Kizayuni unaona kwamba, kusitishwa vita bila ya kufikia malengo yake muhimu ikiwa ni pamoja na kuiangamiza Hamas kuna maana ya kushindwa vitani na kufeli madai yake ya kijeshi na kijasusi. Kwa msingi huo, anasisitiza chaguo la kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Rafah, katika jaribio la kupata pointi na kujiweka katika nafasi bora mkabala wa Hamas katika meza ya mazungumzo.

Jambo lenye muhimu ni kwamba, mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Rafah yatasababisha hali mbaya kwa Ukanda wa Gaza na mji wa Rafah ambao kwa sasa umewapa hifadhi mamia ya maelfu ya Wapalestina.

Kuwepo kwa vikosi vya jeshi la Israel katika kivuko cha Rafah kumepelekea kufungwa kivuko hicho na kuwazuia Wapalestina kusafiri kupitia eneo hilo. Kufungwa kivuko hicho cha mpakani pia kutawaweka wagonjwa wa Kipalestina katika makucha na meno ya mauti katika mazingira ya sasa ya kuporomoka kwa mfumo wa afya wa Ukanda wa Gaza.

 Kwa msingi huo inatupasa kusema kuwa, shambulio la Israel dhidi ya Rafah ni kushindwa kwingine kwa jamii ya kimataifa katika kukomesha mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Gaza na kunazidi kuporomosha chini hadhi jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa.

 

3488265

Habari zinazohusiana
captcha