IQNA

Dunia yalaani mashambulizi mapya ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza

17:02 - March 19, 2025
Habari ID: 3480404
IQNA-Jamii ya kimataifa imebainisha hasira yake baada ya utawala katili wa Israel kuendelea na mashambulizi ya anga dhidi ya Gaza, huku ikivunja makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwa na lengo la kumaliza mzozo wake wa miezi 17 na Hamas.

 Zaidi ya Wapalestina 400, wakiwemo wanawake na watoto, waliuawa Jumanne katika mashambulizi ya Israel jambo ambalo limeibua ghadhabu kote duniani.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na maafisa wa haki za binadamu katika umoja huo, akiwemo Volker Turk, wameelezea mashambulizi hayo kuwa ya kutisha, huku Turk akihimiza kusitishwa haraka vita hivyo. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema mapigano hayo yana athari mbaya kwa watoto milioni moja wa Gaza. UNCIEF pia imetoa wito wa msaada wa haraka kwa ajili ya Gaza na kuutaka utawala wa Israel uheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa.  Umoja wa Ulaya, ukiongozwa na Antonio Costa, mkuu wa baraza la umoja huo, umelaani mashambulizi hayo na kusisitiza umuhimu wa kudumisha mkataba wa kusitisha mapigano.

Nchi nyingi kote duniani, zikiwemo Iran, Jordan, Misri, Qatar, Uturuki, Saudi Arabia, na China, zimebainisha wasiwasi wao kutokana na mashambulizi hayo mapya.

Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameilaumu Marekani kutokana na jinai mpya za Israel huko Gaza. Katika taarifa yake Jumanne, Baghaei amesema kuanza tena uchokozi hatari wa Israel huko Gaza ni  "mwendelezo wa mauaji ya kimbari"  katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Viongozi wa Ulaya, kama vile Keir Starmer wa Uingereza, Annalena Baerbock wa Ujerumani na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, wametaka mapigano yasitishwe mara moja. Waziri Mkuu Giorgia Meloni wa Italia ameonya kuhusu mazungumzo yanayotishiwa, huku Uhispania na Ubelgiji zikitahadharisha kuhusu mzigo wa kibinadamu na ukiukaji wa sheria za kimataifa. Uholanzi imetoa wito wa kusitishwa kabisa mapigano.

China pia imetaka utulivu urejee Gaza huku Russia ikionya juu ya kuenea zaidi hali ya taharuki katika eneo. Mashirika ya haki za kiraia kama Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani, CAIR na mashirika ya haki za binadamu pia yamelaani mashambulizi hayo ya kijinai ya Israel dhidi ya Gaza, huku yakitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za haraka kukomosha jinai hizo.

4272874

captcha