IQNA

Jinai za Israel

Idadi kubwa ya Wapalestina wauawa shahidi katika Ijumaa ya umwagaji damu Gaza

20:48 - May 16, 2025
Habari ID: 3480690
IQNA-Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Ghaza ametangaza leo Ijumaa kwamba ukanda huo ndilo eneo la mauaji ya umati ya kutisha zaidi katika siku za hivi karibuni kiasi kwamba Wapalestina 250 wameuliwa shahidi na Israel katika kipindi cha saa 36 zilizopita pekee.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Gaza pia ametangaza kuwa, zaidi ya watu 150 waliojeruhiwa wamehamishiwa katika hospitali za Al-Awda na Indonesia.

Wizara ya Afya ya Gaza imeeleza kuwa wengi wa majeruhi waliopelekwa hospitalini wamekatika viungo vya miili yao. Taarifa ya Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni unalenga hospitali kwa makusudi, na pia jeshi katili la Israel linaendelea kutumia silaha mpya zilizopigwa marufuku kushambulia vituo vya raia huko Gaza.

Hospitali ya Al-Awda iliyoko Tal al-Za'tar, kaskazini mwa Gaza, imeripoti kupokea mashahidi watano, wakiwemo watoto watatu, na 75 waliojeruhiwa katika mashambulizi ya makombora kwenye nyumba za raia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Vilevile ndege za kivita za Israel zimeendelea kushambulia maeneo ya kusini mashariki mwa Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza na kufanya jinai nyingine kubwa.

Leo asubuhi, jeshi la Israel limeshambulia eneo la mashariki mwa Tel al-Za'tar katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. 

Leo asubuhi pia ndege za kivita za Israel zimeshambulia miji ya Al-Qararah na Khuza'ah, mashariki mwa Khan Yunis kwa mara kadhaa.

Kwa mujibu wa ripoti , tangu utawala haramu wa Israel uanzishe mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza iOktoba 7, 2023, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi imepindukia 53,200 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia 119,998. Aghalabu ya waliouawa au kujeruhiwa ni wanawake na watoto. 

Israel imezidisha jinai zake hizo huku dunia ikiwa katika siku za kukumbuka "Nakba" yaani nakama na janga la tarehe 15 Mei 1948 ambapo Wazayuni walifanya jinai za kutisha mno dhidi ya Wapalestina na kuwalazimisha kuhama kwa nguvu makazi yao ya jadi na baada ya hapo likaundwa dola pandikizi la Israel katika ardhi walizoporwa kinyama Wapalestina.

4282773

Habari zinazohusiana
captcha