IQNA

UNRWA: Waarabu wawape Wapalestina tone tu la Matrilioni waliyompa Trump

19:09 - May 30, 2025
Habari ID: 3480762
IQNA-Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa Linalowahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amezitaka nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi kutenga tone tu la fedha zilizotajwa katika ‘makubaliano makubwa’ kati yao na Rais wa Marekani, Donald Trump, ili kusaidia wakimbizi wa Kipalestina wanaopambana kuendelea kuishi katika ardhi zao ambazo Israel imezikalia kwa mabavu na pia wale wanaoishi katika nchi jirani.

Philippe Lazzarini ameiambia tovuti ya Middle East Eye kwamba UNRWA, mtoaji mkubwa wa msaada kwa wakimbizi milioni sita wa Kipalestina, kwa sasa inakabiliwa na ‘upungufu wa fedha’ ambao huenda ukaibua maamuzi magumu.”

Ameongeza kuwa: “Kwa sababu ikiwa hatuna rasilimali, hatuwezi kuwalipa wafanyakazi. Huenda tukajikuta katika hali ambayo hata mishahara hatuwezi kuandaa. Na ikiwa hali hiyo itatokea, shirika litashurutika kuchambua ni huduma zipi kati ya huduma muhimu ni za dharura zaidi kuliko nyingine.”

Shirika la UNRWA, ambalo wafanyakazi wake wengi ni wakimbizi wa Kipalestina, limekuwa likilengwa na mashambulizi ya Israel tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mwezi Oktoba 2023. Takriban wafanyakazi wake 310 wameuawa na jeshi la Israel katika kipindi cha miezi 19 iliyopita, huku zaidi ya asilimia 80 ya majengo yake yakiharibiwa kabisa.

Lazzarini amezizihimiza nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kuongeza ufadhili kwa UNRWA, akisema angependa kuona mikataba ya matrilioni ya dola waliyoingia na Trump katika ziara yake ya karibuni ikijumuisha pia msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina.

Katika ziara yake Asia Magharibi, Trump alitembelea Qatar, Saudi Arabia, na UAE, ambako mikataba yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 700 ilisainiwa. Ikulu ya Marekani ilitangaza kuwa jumla ya mikataba iliyokubaliwa ilikuwa dola trilioni mbili. Lazzarini amesema: “Natamani  hata tone tu la hizo trilioni zote za dola zilizotangazwa lingewafikia pia wakimbizi wa Kipalestina.”

Amesema kuwa hadi sasa, nchi za Kiarabu hazijatoa ufadhili wowote kwa UNRWA katika mwaka wa 2025. Ametoa wito kwa nchi za Kiarabu  kuwekeza katika shirika hilo sambamba na juhudi za kuunda taifa la Palestina lenye utawala kamili.

Tangu kuanza kwa mashambulizi makubwa ya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 2023, hadi Jumatano tarehe 28 Mei 2025, ikiwa ni siku ya 600 ya vita, maisha ya kiraia katika eneo hilo yameporomoka kabisa chini ya mashambulizi yasiyokoma ya Wazayuni.

Kwa mujibu wa ripoti huru na mashirika ya kimataifa, zaidi ya Wapalestina 54,000 wameuawa katika mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na utawala katili wa Israel, huku wengine 123,000 wakijeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Hii ni hali ya janga la kibinadamu lisilo na mfano wake, likiendelea mbele ya macho ya dunia nzima.

Utawala wa Israel unaendelea kupata msaada wa kijeshi, kiuchumi na kisiasa kutoka Marekani, huku ukiendeleza mauaji ya kimbari, ukandamizaji na uharibifu wa makusudi wa miundombinu ya raia.

4285454/

Habari zinazohusiana
captcha