IQNA

Pep Guardiola asema yanaojiri Gaza yanamuumiza moyoni, asema si suala la itikadi

15:19 - June 11, 2025
Habari ID: 3480823
IQNA – Kocha wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola, ameelezea kwa uchungu hali ya mateso ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, akisema ni jambo linalomuumiza sana kila anapofikiria yanayoendelea katika eneo hilo.

Guardiola alitoa kauli hiyo wakati akipokea digrii ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Manchester, kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya uwanja kwa jiji hilo. Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa kihistoria wa Whitworth Hall, na digrii hiyo ilikabidhiwa na Chansela wa Chuo, Nazir Afzal.

Katika hotuba yake ya kupokea heshima hiyo, Guardiola alisimama kidete kwa ajili ya watu wa Gaza, akilaani kile alichokiita mateso ya wazi yanayoendelea kufanywa na Israel katika vita vinavyoendelea huko Gaza.

Guardiola: “Inaumiza Mwili Wote Kuona Kinachotokea Gaza”

Wakati akisimama kwa ajili ya Gaza na watu wake, kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, alielezea uchungu wake kuhusu matukio yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

“Ni maumivu makali mno tunayoyaona Gaza. Inaniuma mwili mzima. Na hebu nieleweke vizuri ,  hili si suala la itikadi... Hapana. Hili ni kuhusu kupenda maisha, kuhusu kujali jirani yako.”

Guardiola aliendelea kwa hisia: “Labda tunafikiria kwamba kuona wavulana na wasichana wa miaka minne wakiuawa na bomu, au hospitalini,  kwa sababu hospitali hazipo tena — si jambo letu. Tunaweza kujipa moyo kwamba hili si jukumu letu. Lakini tahadhari: wanaofuata wanaweza kuwa wetu. Watoto wa miaka minne au mitano wanaofuata wanaweza kuwa watoto wetu.”

“Samahani, lakini tangu jinamizi hili lilipoanza kwa watoto wa Gaza, kila asubuhi ninapoamka na kuwaona watoto wangu, naingiwa na hofu. Labda picha hii inaonekana kama iko mbali na tulipo sasa. Na unaweza kujiuliza: tunaweza kufanya nini?”

Guardiola pia alisisitiza umuhimu wa kusimama kwa ajili ya haki, hata wakati ambapo dunia hujaribu kutufanya tuketi kimya kwa hofu ya matokeo ya kusema ukweli.

“Kuna hadithi moja ninayoikumbuka. Msitu unawaka moto. Wanyama wote wako katika hofu, wamechanganyikiwa, hawana msaada. Lakini ndege mdogo anaruka kwenda baharini, anarudi tena na tena, akiwa amebeba matone madogo ya maji kwenye mdomo wake mdogo.”

“Nyoka anacheka na kusema: ‘Kwa nini, ndugu? Huwezi kuuzima moto.’ Ndege anajibu: ‘Ndiyo, najua.’ ‘Basi kwa nini unarudia tena na tena?’ Nyoka anauliza tena. Ndege anasema: ‘Nafanya sehemu yangu.’”

Guardiola alihitimisha kwa kusema:

“Ndege huyo anajua hatauzima moto, lakini anakataa kubaki bila kufanya chochote. Katika dunia inayotuambia mara kwa mara kwamba sisi ni wadogo mno kuleta mabadiliko, hadithi hiyo hunikumbusha kwamba nguvu ya mtu mmoja haitegemei ukubwa wa matokeo, bali chaguo , chaguo la kujitokeza, la kutokukaa kimya, la kutotulia wakati inajali zaidi.”

Akizungumzia watoto wake watatu – Maria, Marius na Valentina – Guardiola alisema kwamba kila asubuhi “tangu jinamizi lilipoanza” Gaza, kila anapowaona mabinti zake wawili na mwanawe wa kiume, anakumbuka watoto wa Gaza, jambo ambalo humfanya “kuhisi hofu kubwa sana.” Takriban nusu ya wakazi wa Gaza, ambao ni jumla ya watu milioni 2.3, ni watoto. Tangu tarehe 7 Oktoba, 2023, Israel imeua Wapalestina wasiopungua 55,000 wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina,  angalau watoto 17,400 wameuawa, wakiwemo 15,600 waliotambuliwa rasmi. Wengi zaidi bado wamefukiwa chini ya kifusi na wanahofiwa kuwa wamefariki dunia.

3493406

Habari zinazohusiana
captcha