IQNA

Wairani wajitokeza kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kuunga mkono Palestina

17:01 - March 28, 2025
Habari ID: 3480454
IQNA-Wananchi Waislamu wa Iran kote nchini wamejitokeza kwa mamilioni kushiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, kuonyesha mshikamano na Palestina, na kulaani ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hasa katika Ukanda wa Gaza.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif, Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na Mkurugenzi Mkuu wa kamati ya Intifadha mjini Tehran, alitangaza hapo awali kwamba, mikusanyiko ya kuiunga mkono Palestina nchini Iran itaanza saa nne asubuhi kwa saa za hapa nchini, na yanafanyika katika miji zaidi ya 900 kote nchini.

Waliaondaa maandamano ya hapa Tehran tayari wameanisha barabara kadhaa kuu ambazo zinatumiwa na waandamanaji wa Kiirani wanaotaka kutuma ujumbe kwa jamii ya kimataifa juu ya hali ngumu ya maisha ya Wapalestina, na vile vile kuutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe jinai na dhulma unazowafanyia wananchi hao madhulumu wa Palestina huko Gaza.

Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ilitangazwa na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, kwa shabaha ya kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kupigania ukombozi wa Quds Tukufu. 

Jana usiku, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu yanayofanyika leo Ijumaa ya Machi 28 kote duniani yatakuwa ya aina yake na yana umuhimu mkubwa kuliko miaka iliyopita.

Mikusanyiko hiyo ya hadhara ya Siku ya Quds inafanyika katika nchi nyingi za eneo la Asia Magharibi, zikiwemo Iraq, Yemen na Lebanon. Hali kadhalika, maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yanafanyika katika pembe mbali mbalii za dunia, zikiwemo nchi za Afrika.

Kila mwaka, katika siku hii, maandamano na mikutano mikubwa hufanyika katika nchi tofauti duniani kutangaza mshikamano na watu wanaokandamizwa, hasa watu wa Palestina, ambao wamevumilia jinai na mauaji ya kutisha zaidi katika ulimwengu wa sasa, kwa kipindi cha miezi 16 iliyopita.

Tamko la Imam Khomeini lililenga kuunganisha sauti za watu wanaodhulumiwa duniani kote dhidi ya madhalimu, waovu na wavamizi.

Ulimwengu umejaa dhuluma, na kubwa kuliko yote ni kukaliwa kwa mabavu Palestina kwa zaidi ya miaka 75 na utawala wa kikoloni na unaotenda jinai za kutisha wa Israel.

Utawala huo unaoungwa mkono na nchi za Magharibi, na hasa Marekani, unaendelea kuwachinja bila huruma Wapalestina huko Gaza, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake. Kufikia sasa, zaidi ya watu 50,000 wameuawa tangu Oktoba 7, 2023, kwa mujibu wa takwimu rasmi. Takwimu zisizo rasmi ziko juu zaidi.

Utawala huu muovu umeharibu karibu hospitali na shule zote za Gaza, pamoja na miundombinu ya kiraia katika ukanda huo uliozingirwa, na kuwaua watoto wasio na hatia, madaktari, waandishi wa habari, wasomi na wanaharakati katika juhudi zake za kishetani za kuangamiza kizazi kizima cha Palestina.

/3492519

captcha