Ijumaa, Machi 28, itakuwa Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu. Tukio la kila mwaka hushuhudua maandamano duniani kote katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtakatifu wa Ramadhani.
Katika taarifa, Hamas imewataka Wapalestina na watu duniani kote kuingia mitaani Ijumaa, Jumamosi, na Jumapili katika kutetea Gaza, al-Quds, na Msikiti wa al-Aqsa.
“Maandamano haya pia yana lengo la kusaidia uvumilivu wa watu wetu wa Palestina na kukataa uhalifu unaofanywa na askari wa utawala ghasibu wa Israel na waitifaki wake,” iliongeza taarifa.
Hamas pia imetoa wito wa kutumia “njia zote za shinikizo kuzuia mauaji, kuzingirwa, na njaa katika Gaza na kuimarisha uthabiti wa Wapalestina katika Yerusalemu na Msikiti wa al-Aqsa.”
Jeshi la utawala wa Israeli ulianza mashambulizi mapyai ya angani ya kushangaza kwenye Ukanda wa Gaza tarehe 18 Machi, likiua zaidi ya watu 730 na kujeruhi karibu 1,200 wengine licha ya makubaliano ya kusitisha vita na kubadilishana wafungwa yaliyoshikiliwa tangu Januari.
Zaidi ya Wapalestina 50,000 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na zaidi ya 113,400 kujeruhiwa katika mashambulizi makali ya kijeshi ya Israeli dhidi ya Gaza tangu Oktoba 2023.
Zaidi ya Wapalestina 930 pia wameuawa katika mashambulizi ya jeshi la Israeli na walowezi wasiokuwa halali katika Ukingo wa Magharibi na Mashariki ya al-Quds katika kipindi hicho hicho.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa hati za kukamatwa mwezi Novemba uliopita kwa waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Gaza.
Israeli pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa vita vyake dhidi ya eneo hilo.
Inafaa kuashiria hapa kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa urithi wa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Ammrehemu), ambaye anaheshimiwa kama kiongozi wa kiroho na Waislamu duniani kote.
Mnamo mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalimpindua mtawala wa kiimla, Shah, aliyeungwa mkono na Marekani pamoja na Israel, Imam Khomeini aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa Quds ili Waislamu na wapenda haki kote duniani waweze kujitokeza katika siku hiyo katika maandamano na mijumuiko ya kuunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina sambamba na kulaani utawala wa Kizayuni wa Israel unaozikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Mji wa al-Quds (Jerusalem) unachukuliwa kuwa nembo ya ukombozi wa Palestina kwani unatazamiwa kuwa mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.
4273617