
Kwa ushiriki mkubwa wa wananchi, ujumbe wa muqawama (mapambano ya Kiislamu ya kusimama imara) na kutangaza upya ahadi ya utiifu kwa malengo ya kiongozi huyo shahidi na Mapinduzi ya Kiislamu umetumwa kwa ulimwengu. Washiriki pia wamewafahamisha wavamizi wakuu, yaani Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na wanaowaunga mkono: “Tutaendelea kumwadhibu adui hadi tone la mwisho la damu.”
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, sambamba na kuwadia kwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, hafla kubwa ya maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds imefanyika leo asubuhi, Ijumaa mjini Tehran na katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Maandamano haya, ambayo ni alama ya umoja wa Umma wa Kiislamu katika kuunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani uhalifu unaoendelea wa utawala vamizi wa Kizayuni wa Israel, mwaka huu yamefanyika kwa hisia na umakini mkubwa zaidi, katika mazingira ambayo Iran inaendelea kushambuliwa kijeshi na Marekani na utawala wa Kizayuni Israel. Vita hivyo vilianza Februari 28 sawa na tarehe 10 Ramadhani.
Haya ndiyo maandamano ya kwanza ya Siku ya Quds kufanyika bila uwepo wa kiongozi shahidi Imam Khamenei, ambaye daima alikuwa mstari wa mbele kupaza sauti kwa ajili ya malengo ya Palestina na kuahidi kuja kwa ukombozi wa Quds pamoja na kutoweka kwa utawala wa Kizayuni. Kwa hivyo, mahudhurio haya makubwa ya wananchi yanaelezwa kuwa ni kufanya upya kiapo cha uaminifu kwa kiongozi huyo shahidi wa taifa la Iran, pamoja na kusisitiza azma ya wananchi ya kuendelea kufuatilia lengo la ukombozi wa Palestina.
Matukio makubwa
Maandamano haya, kutokana na matukio makubwa yanayoendelea katika eneo la Asia Magharibi ( Mashariki ya Kati) na pia mashambulizi ya hivi karibuni ya kile kinachoitwa mfumo wa ubeberu pamoja na utawala wa Kizayuni dhidi ya mipaka ya nchi yetu, yalibeba uzito maalum wa kihisia na kiroho. Njia zinazoelekea Chuo Kikuu cha Tehran zilishuhudia umati mkubwa na wa hiari wa makundi mbalimbali ya wananchi. Licha ya nchi kuwa katika mazingira ya vita, vitisho vya maadui na pia hali ya kiroho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, watu walijitokeza wakiwa wamekunja ngumi zao na macho yenye machozi kwa huzuni ya kumpoteza kiongozi wa taifa, lakini wakiwa na matumaini kwa siku zijazo, wakipaza sauti kwa pamoja kauli mbiu za “Kifo kwa Israel” na “Kifo kwa Marekani.”

Ndege za kivita za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zimedondosha mabomu wakati maandamano hayo yakiendelea lakini hilo halikuwazuia wananchi kutoa nara dhidi ya tawala hizo mbili za kigaidi.
Washiriki wa tukio hili kubwa la kihistoria walibeba picha za mwanzilishi mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhollah Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu), pamoja na kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mrithi wake, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei. Washiriki walitangaza upya ahadi yao ya utiiifu kwa malengo ya juu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mashahidi wake watukufu. Hali hii inaonesha kwamba maandamano haya yamekuwa uwanja wa kudhihirisha hamasa ya kidini na ya kitaifa, huku ushiriki wa vizazi mbalimbali vya waandamanaji ukiwa ishara ya umoja na mshikamano wao katika kuunga mkono azma ya Palestina.
Tutaendelea kumwadhibu adui hadi tone la mwisho la damu
Waandamanaji waliokuwa katika Saumu ya Ramadhani, huku wakitangaza kuchukizwa na uhalifu wa Marekani na utawala wa Kizayuni—iwe ndani ya Iran au katika Ukanda wa Gaza na Lebanon—walitoa pia wito mkali kwa viongozi wao wa kiraia na wa kijeshi kuendelea na njia ya heshima ya muqawama na kuwachukulia hatua kali wavamizi. Uwepo mkubwa wa wananchi katika maandamano haya ulipeleka ujumbe wazi kwa wavamizi wa Marekani na Kizayuni pamoja na wanaowaunga mkono: “Tutaendelea kumwadhibu adui hadi tone la mwisho la damu.”

Siku ya Quds ya mwaka huu kwa hakika iligeuka kuwa uwanja wa tukio kubwa ambalo lilionekana kama pigo la wananchi dhidi ya taghuti. Wananchi walionekana wakikanyaga bendera za ubeberu , yaani Marekani na Israel, huku wakipaza sauti kwa nguvu kauli mbiu ya “Mauti kwa Marekani,” na “Mauti kwa Israel”.
Viongozi wa Iran katika maandamano
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria maandamano hayo walikuwa Rais Masoud Pezeshkian; Mkuu wa Idara ya Mahakama, Hujjat al‑Islam wal‑Muslimin Gholamhossein Mohseni Ejei; Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, Ali Larijani; mshauri na msaidizi maalum wa kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mohammad Mokhber; Waziri wa Mambo ya Nje, Sayyid Abbas Araghchi; mkuu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia, Mohammad Eslami; Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu, Sayyid Abbas Salehi; Meya wa Tehran, Alireza Zakani; Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara, Sayyid Mohammad Atabak; Waziri wa Elimu, Alireza Kazemi; Waziri wa Michezo na Vijana, Ahmad Donyamali; Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji, Farzaneh Sadegh; Mwenyekiti wa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo, Ayatullah Amoli Larijani; na Waziri wa Mafuta, Mohsen Paknejad.
Taarifa ya mwisho
Mwisho wa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, waandamanaji walitoa tamko rasmi ambapo sambamba na kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Palestina, wametangaza bay‘a au kiapo cha utiifu kwa kiongozi mpya wa Mapinduzi, huku wakisisitiza ulazima wa “kuwaadhibu wavamizi” na kulipiza kisasi kwa damu ya shahidi Imam Khamenei pamoja na mashahidi wa tukio la kigaidi katika shule ya Minab.
Katika sehemu ya tamko hilo imesema: “Sisi, wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walio waaminifu kwa Wilayat Faqhi (Faqihi Mtawala), katika maandamano haya makubwa na ya kihistoria, tunapaza sauti kwa pamoja tukitangaza kwamba tumesimama imara juu ya ahadi na kiapo chetu kwa malengo ya juu ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na Imam shahidi Khamenei (Mwenyezi Mungu amrehemu). Kwa nyoyo zilizojaa mapenzi na kwa azma thabiti kama chuma, tunafanya upya bay‘a yetu kwa nahodha wa tatu wa jahazi la Mapinduzi, kiongozi mwenye hekima na busara wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde), na tunatangaza kwamba tutasimama imara juu ya ahadi na kiapo chetu kwa Wilayah hadi tone la mwisho la damu.”
4340335