Kwa mujibu wa Urais Mkuu wa Masuala ya Msikiti Mtakatifu wa Makka na Msikiti wa Mtume (SAW), hatua hii ni sehemu ya taratibu za kawaida za kuwapokea mahujaji kwa msimu wa Hija wa mwaka 1446 Hijria.
Mchakato huo unahusisha kukunja na kufunga sehemu ya chini ya Kiswah, kuiinua hadi mita tatu kutoka ardhini, kisha kufunika sehemu iliyo wazi kwa kitambaa cheupe cha pamba chenye upana wa takriban mita mbili.
Desturi hii ya kila mwaka hufanywa ili kulinda Kiswah dhidi ya kuguswa au kuharibika wakati wa Hija, hasa kutokana na idadi kubwa ya waumini wanaofanya Tawaf (ibada ya kuizunguka Kaaba).
Kuinyanyua Kiswah kunasaidia kuhifadhi uimara na heshima ya kitambaa hicho katikati ya misongamano ya Mahujaji.
Timu maalumu za kitaalamu huendesha shughuli hii kwa kufuata viwango vya usalama na kwa heshima ya hali ya juu kwa utakatifu wa eneo hilo.
Kaaba, iliyoko katikati ya Msikiti Mtakatifu wa Makka, ndiyo mahali patakatifu zaidi katika Uislamu na kitovu cha ibada ya Hija, ambayo huvutia mamilioni ya Waislamu kutoka kila kona ya dunia kila mwaka.
3493088