Ayatullah Seyyed Ali Khamenei alitoa matamshi hayo Jumanne wakati wa hafla katika jijini Tehran, kuadhimisha hauli ya kwanza ya kufa shahidi Ebrahim Raisi.
Rais Raisi na maafisa kadhaa waandamizi, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, walikufa shahidi katika ajali ya helikopta mnamo Mei 19, 2024, katika Mkoa wa Azarbaijan Mashariki. Helikopta aina ya Bell 212 ilipotea kwenye rada wakati wa safari kutoka kwenye uzinduzi wa bwawa, huku kukiwa na ukungu mzito.
Ayatullah Khamenei amezungumza kuhusu tabia na mtindo wa uongozi wa Raisi, akisema, "Raisi hakujiona kuwa bora kuliko watu," na akasisitiza kuwa "alijiona kuwa katika daraja sawa na watu, na hata chini yao."
Alimsifu Raisi kwa kuwa na "moyo mnyenyekevu," "hotuba ya dhati na ya moja kwa moja," na "matendo yasiyokoma na yenye bidii," kama sifa zilizomwelezea wakati wa uongozi wake.
"Kiburi, kudharau watu, na kuweka mzigo wa uongozi kwa watu ni tabia za utawala wa kifarao," Ayatullah Khamenei alisema. "Raisi alisimama kinyume kabisa na tabia hizo. Aliendesha nchi kwa mtazamo uliomweka katika kiwango cha watu—au hata chini yao."
Alielezea kukataa kwa Raisi kutumia nafasi yake ya kisiasa kwa manufaa binafsi na kujitolea kwake kuwahudumia wengine kama "funzo kubwa." "Kuna watu wengi katika mfumo wa Kiislamu wenye sifa hizi," Kiongozi aliongeza."Lakini maadili haya na masomo haya lazima yawe sehemu ya utamaduni wetu wa kitaifa."
Ayatullah Khamenei pia aligusia uaminifu na uwazi wa kimaadili wa Raisi, akilinganisha na baadhi ya viongozi wa Magharibi. "Ili kuelewa thamani ya uaminifu wake," alisema, "mtu lazima aulinganishe na hotuba za udanganyifu za maafisa katika baadhi ya nchi za Magharibi, wale wanaodai kwa sauti kubwa kutetea amani na haki za binadamu, huku wakifumbia macho mauaji ya zaidi ya watoto 20,000 wasio na hatia huko Gaza na kuwasaidia wahalifu."
Hafla hiyo ya kumbukumbu ilihudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu, wakiwemo wakuu wa matawi ya utawala wa Iran pamoja na familia za mashahidi na wananchi.
Miongoni mwa washiriki walikuwa watoto wa shhahidi Sayyed Hassan Nasrallah, aliyekuwa kiongozi wa Hezbullah, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la Israeli huko Beirut mwaka jana.
Katika siku zilizotangulia kumbukumbu hiyo, viongozi wa ndani na wa kimataifa walitoa heshima kwa urithi wa Raisi, wakikumbuka kujitolea kwake kwa haki ya kijamii, maadili ya kidini, na huduma kwa umma.
Kadhia ya nyuklia
Wakati huo huo, akizungumza katika hafla hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Iran haingojei ruhusa ya mtu yeyote ili kurutubisha madini ya urani na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ina sera zake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Tulizungumzia kuhusu mazungumzo, na ningependa kutoa onyo kwa upande wa pili: Upande wa Marekani ambao unashiriki katika mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja, lazima uache kutoa kauli za kipumbavu."
Ayatullah Khamenei amesema: Upande mwingine [wa mazungumzo] unasema kwa ujeuri kabisa kwamba, hatutaruhusu Iran kurutubisha madini ya urani. Hakuna anayesubiri ruhusa kutoka upande wowote." Jamhuri ya Kiislamu ina sera na misingi na inafuata sera yake yenyewe.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Nitawaeleza wananchi wa Iran katika tukio na mnasaba mwingine maudhui ya kurutubisha madini ya urani, na kwa nini Wamagharibi, na hasa Wamarekani wanashikilia sana kuzuia urutubishaji nchini Iran. Nitashughulikia masuala haya, Mwenyezi Mungu akipenda, katika tukio la baadaye ili wananchi wa Iran wajue nini makusudio ya upande mwingine [wa mazungumzo]."
3493167/l