IQNA

Kadhia ya Palestina

Kikao cha OIC cha mjini Jeddah chajadili kadhia ya kuuawa shahidi Ismail Haniya

17:26 - August 08, 2024
Habari ID: 3479245
IQNA-Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imeamua kuitisha kikao dha dharura mjini Jeddah, Saudi Arabia wakati huu ambapo Iran na kambi ya muqawama inajiandaa kutoa majibu makali kwa Israel kutokana na vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni.

Ali Bagheri, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jana Jumatano asubuhi aliondoka mjini Tehran kuelekea Jeddah, akiongoza ujumbe wa Iran kwa ajili ya kushiriki katika kikao hicho cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC. Kikao hicho cha OIC ni cha kujadili matokeo mabaya ya jinai za Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na vilevile jinai ya utawala haramu wa Kizayuni ya kumuua shahidi Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Jinai nyingine ya Israel ni kuvunja haki ya kujitawala taifa la Iran kwani Ismail Haniyeh ameuliwa kigaidi na utawala wa Kizayuni ndani ya ardhi ya Iran tena akiwa mgeni rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kikao hicho cha dharura cha OIC ni matunda ya juhudi kubwa na amilifu za kidiplomasia za Iran kwani Tehran ndiyo iliyopendekeza Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC wakutane katika kikao cha dharura kujadili jinai za Israel na kutafuta njia za kukomesha ukatili wa utawala wa Kizayuni na masuala mengine ya kieneo na kimataifa. 

Katika kikao hicho kisicho cha kawaida cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu alitathmini hatua ya utawala wa Kizayuni katika kumuua shahidi Ismail Haniya, kama ukiukaji wa uhuru na mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hossein Ebrahim Taha, Katibu Mkuu wa OIC katika hotuba yake katika kikao kisicho cha kawaida cha Kamati ya Utendaji ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jumuiya hiyo mjini Jeddah alisema: Sisitizo la utawala ghasibu wa Israel kuhusu jinai ni ukiukaji wa miiko yote, desturi, sheria na maazimio ya kimataifa.

Wajibu wa nchi za Kiislamu baada ya kuuawa shahidi Haniya

Baada ya utawala wa Kizayuni kumuuua kidhulma shahid Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifanya mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia na Qatar na huku akigusia wajibu wa nchi za Kiislamu wa kuitisha kikao cha dharura cha kuzungumzia kuuawa shahidi Ismail Haniya alipendekeza pia kikao hicho kifanyike haraka mjini Jeddah, Saudi Arabia katika kiwango cha mawaziri wa mambo ya nje.

Kikao hicho cha dharura cha OIC kimefanyika mjini Jeddah katika hali ambayo utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya jinai dhidi ya wananchi wa Palesitna hasa wa Ukanda wa Ghaza kiasi kwamba hivi sasa zaidi ya wananchi 40,000 wa Palestina wameshauawa shahidi na 91,000 wengine wameshajeruhiwa kutokana na jinai hizo za miezi 10 za Wazayuni. Asilimia kubwa ya wahanga hao ni wanawake na watoto wadogo. Zaidi ya nyumba 43,000 za Wapalestina zimeshabomolewa na miundombinu pamoja na huduma za afya na matibabu, Misikiti na sehemu za ibada, maeneo ya historia na kila sehemu imeharibiwa na utawala katili wa Israel huko Ghaza. 

Iran, Saudi Arabia katika mkondo mzuri

Hivi sasa nchi mbili kubwa za Ulimwengu wa Kiislamu yaani Iran na Saudi Arabia zimeingia kwenye mkondo mzuri wa kuwa na uhusiano unaostawi, kushirikiana katika masuala mbalimbali na kuwa na mikakati ya pamoja kwa ajili ya usalama na amani katika ukanda huu. Lakini utawala wa Kizayuni ambao tangu kuasisiwa kwake umeasisiwa juu ya msingi wa kutenda jinai na kufanya ukatili wa kuchupa mipaka, haifurahishwi hata kidogo na kuona eneo hili lina utulivu; na muda wote Israel inafanya jinai na uhalifu usioelezeka kwa maneno, ili upate kisingizio cha kuwepo kwake katika eneo hili. 

Baadhi ya watu wanasema kuwa, utawala wa Kizayuni umefanya jinai kubwa hivi karibuni za kuwaua shahidi makamanda wa Muqawama nchini Iran na Lebanon na vile vile kushambulia al Hudaidah huko Yemen ili kambi ya muqawama itoe majibu makali ambayo yatafanikisha lengo la Benjamin Netanyahu, waziri mkuu nduli wa utawala wa Kizayuni yaani lengo la kuzusha vita vya eneo hili zima kwani ni kwa kufanya hivyo ndipo ataweza kubakia madarakani kwa kisingizio cha kukabiliana na maadui wa Israel. Lakini wachambuzi wengine wanasema kuwa, iwapo kambi ya muqawama haitotoa majibu makali dhidi ya utawala wa Kizayuni, basi Wazayuni watapata kiburi cha kufanya mauaji mengine na watapata uthubutu mkubwa zaidi wa kuvuuka mistari myekundu ya kambi ya muqawama. 

Hivi sasa imethibitika wazi zaidi kwamba lengo la utawala wa Kizayuni ni kuwaondoa kabisa Wapalestina Waarabu katika ardhi zao zote za Palestina; si Ukanda wa Ghaza tu, bali pia wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pamoja na hata wale wanaoishi katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel.

Msimamo wa pamoja

Ni wazi kwamba, iwapo nchi za Kiislamu kupitia OIC ambayo iliasisiwa kwa ajili ya kukiunga mkono Kibla cha Kwanza cha Waislamu ya Msikiti wa al Aqsa, wataweza kuchukua msimamo wa pamoja kwa kuzingatia hali hiyo halisi ya mambo na malengo hayo machafu ya Israel, basi bila ya shaka yoyote utawala wa Kizayuni si tu hautoweza kufikia ndoto yake ya kuziteka ardhi zote za Palestina na kuunda dola la Kizayuni, lakini pia utalazimika kukomesha jinai zake huko Palestina na hasa Ukanda wa Ghaza. Kukosekana umoja na mshikamano katika safu za Waislamu ndicho kikwazo kikubwa cha kufikiwa malengo matukufu ya Waislamu hasa ukombozi wa Quds ambayo ndiyo kadhia kuu zaidi ya Waislamu wote. 

4230691

423070

Habari zinazohusiana
Kishikizo: shahidi ismail haniya
captcha