IQNA

Rais wa Ebrahim Raisi wa Iran

Iran itazisaidia nchi za Afrika kupata teknolojia mpya

17:35 - March 08, 2023
Habari ID: 3476678
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran iko tayari kuzipatia nchi za Afrika elimu na teknolojia mpya ili kurahisisha ushiriki wa sekta binafsi katika uhusiano wa pande mbili.

Rais wa Iran aliyasema hayo Jumatatu jioni mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na washiriki wa 'Kikao cha Kwanza cha Ushirikiano wa Sayansi na Uchumi kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Nchi za Afrika Magharibi.' Raisi amesisitiza kuwa Iran iko tayari kuimarisha uhusiano na nchi zote za Afrika hasa nchi za Magharibi mwa Afrika. Katika kikao hicho, Raisi amesema Afrika ni bara tajiri ambalo lina nguvu kazi yenye uwezo pamoja na utajiri mkubwa wa akiba ya mali asili.

Aidha amesisitiza kuwa, kustawishwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Afrika ni kwa lengo la ustawi na maendeleo ya mataifa yote ya Afrika.

Aidha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuhusu umuhimu wa kufahamu uwezo, vyanzo na nyuga za ushirikiano sambamba na kubadilishana uzoefu baina ya Iran na nchi za Afrika Magharibi. 

Rais wa Iran ameashiria ustawi mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga za uhandisi, vifaa vya tiba, dawa, teknolojia ya nano, mashine za kilimo, biolojia, sayansi na teknolojia mpya. Amesema Iran imepata ustawi huo pamoja na kuwepo vikwazo vingi dhidi yake na kuongeza kuwa: "Iran iko tayari kuzipatia nchi zinginezo zikiwemo za Afrika elimu na teknolojia mpya."

Raisi aidha amesema Iran na Afrika zinakabiliana na vitisho vya pamoja kupitia makundi ya kigaidi yanayopata himaya ya ajinabi na madola makubwa yaliyo nje ya eneo na kuongeza kuwa: "Afrika ina uwezo mkubwa wa nguvu kazi na mali asili na kwa mshikamano na umoja bara hili linaweza kukabiliana na madola ya kibeberu na hivyo kupata maendeleo makubwa.

Rais wa Iran pia amesema,  "Katika karne zilizopita, nchi za Magharibi zilipora utajiri wa nchi za Kiafrika kwa kuanzisha utawala wa kikoloni."

Mkutano wa siku tatu wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Sayansi na Uchumi baina ya Iran na nchi za Afrika Magharibi ulianza jana Jumatatu hapa mjini Tehran. Mawaziri, mabalozi na wawakilishi wa sekta za biashara, nishati na viwanda wa Iran na nchi za Afrika Magharibi wanahudhuria mkutano huo wa siku tatu.

Akihutubu katika kikao hicho, Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kusainiwa hati 20 za ushirikiano katika nyuga tofauti zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na kiutalii katika siku ya kwanza ya mkutano huo baina ya Jamhuri ya Kiislamu na mataifa hayo ya Afrika kunaonesha azma na irada ya kisiasa ya pande mbili ya kuimarisha uhusiano na maingiliano yao.

4126615

captcha