Semina hiyo imeandaliwa na Shirika la Habari za Qur’ani la Kimataifa (IQNA) ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya mwaka wa 36 tangu kufariki kwa, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu) muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Itaanza saa tatu asubuhi kwa saa za Iran (saa 11:30 alfajiri GMT) na itatangazwa mubashara kupitia tovuti: aparat.com/iqnanews/live. Mzungumzaji mkuu katika semina hiyo atakuwa Hujjatul Islam Seyed Mostafa Hosseini Neyshabouri, Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Qur’ani na Uenezaji wa Kiislamu, kilicho chini ya Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu. Atazungumzia mada “Imamu Khomeini (RA); Mrekebishaji Mkuu wa Dunia ya Kisasa.” Miongoni mwa wachangiaji wengine watakuwa ni wanazuoni kutoka Bahrain, Iraq na Lebanon. Sheikh Abdullah Daqqaq, mwanazuoni kutoka Bahrain, atatoa mada kuhusu “Hija na Maendeleo ya Harakati ya Kifikra ya Ulimwengu wa Kiislamu katika Mtazamo wa Imamu Khomeini (RA).” Jumaa Al-Otwani, Mkurugenzi wa Kituo cha “Horizon” cha Utafiti wa Kisiasa mjini Baghdad, Iraq, atatoa muhadhara wa video kuhusu “Imamu Khomeini (RA) na Mkakati wa Umoja wa Kiislamu.” Linda Taboush, mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya kijamii kutoka Lebanon, atawasilisha mada yake juu ya “Imamu Khomeini (RA): Mvumbuzi wa Utambuzi wa Nafsi wa Umma wa Kiislamu.” Ayatullah Ruhollah Moussavi Khomeini, maarufu kama Imam Khomeini, ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979, ambayo yalimaliza utawala wa kifalme wa Shah aliyekuwa kibaraka wa Marekani. Imam Khomeini alizaliwa mwaka 1902 na akawa kiongozi mashuhuri wa harakati za wananchi wa Iran katika miaka ya 1970 dhidi ya mfumo wa kifalme wa karne nyingi. Imamu Khomeini alifariki dunia tarehe 3 Juni 1989 akiwa na umri wa miaka 87. 3493308