IQNA

Saudia imeanza tena utoaji wa Visa za Umrah

17:56 - June 10, 2025
Habari ID: 3480820
IQNA – Maombi ya visa za Umrah yameanza tena rasmi siku ya leo Jumanne, tarehe 10 Juni, hivyo kuwapa fursa waumini kutoka mataifa mbalimbali kuanza maandalizi ya safari tukufu kuelekea miji mitakatifu ya Makkah na Madinah kwa ajili ya Hija ndogo ya Umrah.

Wizara ya Hija na Umrah ya Saudi Arabia imethibitisha uzinduzi wa msimu mpya wa Umrah, huku vikundi vya kwanza vya 'Mahujaji wa Umrah' kutoka nje ya nchi vikitarajiwa kuwasili Jumatano, tarehe 11 Juni.

Tofauti na Hija ambayo hufanyika katika mwezi wa Dhul Hija, Umrah, ambayo pia huitwa 'Hija Ndogo'  hufanyika wakati wowote wa mwaka.

Kwa mujibu wa ratiba ya wizara, watoa huduma na mawakala wa kimataifa walitakiwa kukamilisha makubaliano ya ushirikiano kufikia tarehe 27 Mei.

Kurejelewa kwa utoaji wa Visa kunakuja baada ya kukamilika kwa ibada ya Hija ya mwaka huu, ambayo imewakutanisha zaidi ya Mahujaji milioni 1.6 kutoka pembe zote za dunia. Baadhi yao tayari wameanza kurejea makwao, huku wengine wakiendelea na safari hadi Madinah.

Kwa kawaida, utoaji wa Visa za Umrah husimamishwa kwa muda mfupi kabla ya Hija ya kila mwaka, ili kuruhusu usimamizi wa rasilimali kwa maandalizi ya ibada ya Hija ambayo huhusisha idadi kubwa ya Mahujaji kwa kipindi kifupi.

/3493396

captcha