IQNA

Jinai ya Israel

Makamanda Waandamizi wa Iran, akiwemo Jenerali Salami, wauawa shahidi katika hujuma ya Israel

6:57 - June 13, 2025
Habari ID: 3480827
IQNA-Meja Jenerali Hossein Salami, kamanda mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), pamoja na Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran wameuawa shahidi katika hujuma ya anga lililotekelezwa na utawala katili wa Israel mapema Ijumaa alfajiri mjini Tehran.

Ripoti pia zinaeleza kuwa maafisa wengine waandamizi wa IRGC na wanasayansi wa nyuklia kadhaa wamekuwa miongoni mwa mashahidi katika mashambulizi hayo yaliyoilenga Tehran na mikoa mbalimbali nchini Iran.

Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, IRIB, limethibitisha kuwa Meja Jenerali Gholam Ali Rashid, kamanda mwandamizi katika Kamandi ya Majeshi ya Iran, pia ameuliwa shahidi katika mojawapo ya mashambulizi hayo.

Wanasayansi waliobobea wa nyuklia, Mohammad-Mehdi Tehranchi na Fereydoon Abbasi, pia wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya alfajiri ya leo.

Mashambulizi ya kwanza yaliripotiwa karibu saa tisa usiku kwa saa za Tehran siku ya Ijumaa, yakifuatiwa na milipuko mingine katika mikoa kadhaa nchini kote.

Video zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo ya makazi jijini Tehran na sehemu nyingine, matokeo ya kile kilichoelezwa kuwa ni uvamizi wa kiholela uliofanywa na utawala wa Israel.

Utawala haramu wa Israel umethibitisha kuhusika na mashambulizi hayo, ukidai kuwa ulilenga maeneo ya Natanz, Khorramabad, Khondab, pamoja na maeneo mengine kadhaa.

Shirika la habari la IRNA, likimnukuu chanzo cha usalama, limesema kuwa Iran inajiandaa kutoa "jibu kali na la wazi" dhidi ya kitendo hiki cha kigaidi kilichofanywa na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Uvamizi huu unakuja katika kipindi cha mvutano mkali unaoendelea kuongezeka katika ukanda wa Asia Magharibi, ukichochewa na matamshi ya kichochezi kutoka kwa viongozi wa utawala wa Israel, akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Inaripotiwa kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, alitoa idhini kwa mashambulizi haya ya Israel licha ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kati ya Tehran na Washington.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, duru ya sita ya mazungumzo hayo iliyopangwa kufanyika Jumapili huenda ikafutwa.

3493429

 

Kishikizo: Ahadi ya Kweli Salami
captcha