IQNA

Operesheni kubwa ya kijeshi ya Iran dhidi ya Israel yafanikiwa

10:48 - June 14, 2025
Habari ID: 3480831
IQNA-Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeanza kutekeleza wimbi la mashambulizi ya makombora dhidi ya utawala waKizayuni Israel, ili kulipiza kisasi kufuatia hujuma za utawala huo wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Iran.

Afisa mkuu wa kijeshi wa Iran amethibitisha kuwa Iran ililenga zaidi ya maeneo 150 katika shambulio lake la kulipiza kisasi dhidi ya Israel, ikigonga vituo vingi vya kijeshi vya thamani kubwa.

Katika mahojiano ya mapema Jumamosi na televisheni ya taifa ya Iran, Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi, mshauri mkuu wa kamanda mkuu wa IRGC, alitangaza utekelezaji wa mafanikio wa operesheni hiyo ya hatua nyingi. “Malengo haya yaligongwa kwa mafanikio katika hatua kadhaa,” alisema Vahidi, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani chini ya Shahidi Rais Ebrahim Raeisi.

Jenerali huyo alifafanua maeneo kadhaa muhimu yaliyoshambuliwa, ikiwa ni pamoja na Kituo cha Anga cha Nevatim katika eneo la kaskazini-kati na Kituo cha Anga cha Ovda kusini mwa maeneo yaliyochukuliwa. Alieleza kuwa vituo hivyo vilikuwa na sehemu za amri, udhibiti, na vita vya kielektroniki, ambazo alisema zilihusika moja kwa moja katika kuzindua mashambulizi dhidi ya Iran.

Vahidi pia alitaja Kituo cha Anga cha Tel Nof, kilicho karibu na Tel Aviv, kama lengo jingine muhimu. Aidha, alibainisha kuwa wizara ya masuala ya kijeshi ya Israel pamoja na maeneo ya viwanda vya kijeshi yalilengwa katika kampeni hiyo ya kulipiza kisasi.

Awami hii ya tatu ya operesheni ya kijeshi ya kulipiza kisasi ya Iran - Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3 - ilianza mwendo wa saa saba na nusu usiku wa kuamkia leo kwa saa za hapa Iran, baada ya awamu mbili zenye mafanikio, ambapo maeneo mengi ya kimkakati ya Israel yalilengwa.

Shirika la habari la IRNA limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, Israel imeanza kuhisi ghadhabu ya Iran usiku wa kuamkia leo, wakati Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilipoanzisha wimbi la mashambulizi dhidi ya utawala huo haramu.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari vya Israel, katika wimbi hili jipya, makombora ya Iran yamepiga maeneo tofauti mjini Tel Aviv, Jerusalem (al-Quds), Ziwa Tiberias, Haifa, Beersheba na maeneo mengine.

Uharibifu mkubwa zaidi umeripotiwa Tel Aviv, ambapo angalau kombora moja lilipiga jengo la orofa 50, na kusababisha mripuko mkubwa ambao ulipelekea wingu jeusi la moshi kutanda angani. Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zimeelezea kujiri matukio ya purukushani na wahaka huko Tel Aviv, huku huduma za dharura hasa kusini mwa mji huo zikihangaika huku na kule kuwahudumia majeruhi.

Kutokana na hali nyeti ya maeneo yaliyolengwa, kikosi cha jeshi la Israel kinachojiita 'Home Front Command' kimeripotiwa kulazimisha vyombo vya habari kuzima au kuchuja baadhi ya habari ili kuepusha aibu zaidi.

Katika taarifa ya pili baadaye saa sita usiku, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilisema vitengo vya makombora na ndege zisizo na rubani vililenga kambi za jeshi la Israel ambazo zilitumiwa kuanzisha mashambulio dhidi ya Iran, pamoja na utengenezaji wa silaha za kiviwanda na maeneo mengine ya kijeshi ndani ya Israel.

Taarifa hiyo imesema kuwa, taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa, ikiwa ni pamoja na picha za satelaiti, zilionyesha makumi ya makombora ya balestiki ya Iran yalikuwa yamelenga shabaha zao kwa usahihi.

3493435

 

captcha