IQNA

Ayatullah Khamenei: Majeshi ya Iran yataupiga kwa nguvu utawala wa kigaidi na kishetani wa Israel

19:17 - June 14, 2025
Habari ID: 3480833
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema kuwa Vikosi vya Ulinzi vya Iran vitachukua hatua kali na kuufanya utawala wa Kizayuni wa Israel ufedheheke.

Ayatullah Khamenei alituma ujumbe maalum kwa taifa la Iran siku ya Ijumaa usiku, kufuatia mashambulizi ya kichokozi yaliyofanywa na Israel dhidi ya maeneo mbalimbali ya Iran.

Ifuatayo ni hotuba kamili ya Imam Khamenei iliyotolewa kupitia televisheni kufuatia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika maeneo mbalimbali ya Iran na kuuawa shahidi kwa kundi la makamanda, wanasayansi na raia mnamo tarehe 13 Juni 2025.

 

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Nawasalimu wananchi wetu wapendwa na waungwana wa taifa hili. Natuma salamu zangu za pongezi na rambirambi kwa taifa la Iran na familia za mashujaa wetu waliouawa shahidi, wakiwemo makamanda wapendwa, wanasayansi na raia wa kawaida. Bila shaka, huu ni msiba mzito kwa kila mmoja wetu. Tunatarajia, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, kwamba daraja zao zitainuliwa na roho zao safi zipate fadhila maalum za Mola.

Ninachotaka kusema kwa taifa letu tukufu ni kwamba utawala wa Kizayuni umefanya kosa kubwa, kosa ambalo ni hatari, na kitendo cha kiholela. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, matokeo ya kosa hilo yatausambaratisha utawala huo dhalimu. Taifa la Iran halitaruhusu damu ya mashahidi wake wenye thamani kumwagika bila kisasi, wala halitakubali ukiukaji wa anga yake ya taifa kupita kimya kimya.

Majeshi yetu yako tayari. Viongozi wa taifa na wananchi wote wamesimama kidete kuunga mkono majeshi ya Iran. Leo hii, kutoka pande zote za kisiasa na makundi mbalimbali ndani ya nchi, sauti zimeungana. Kila mmoja anatambua umuhimu wa kujitokeza na kutoa jibu thabiti dhidi ya utawala huu wa kigaidi, wa kishetani, na wenye kuchukiza.

Lazima tutoe jibu la nguvu. InshaAllah, tutajibu kwa nguvu, na hatutawahurumia. Hakika maisha yatawageukia kuwa machungu. Wasidhani kuwa wameshambulia na kila kitu kimemalizika. Hapana! Wao ndio walioanzisha haya, wao ndio waliotangaza vita.

Utawala wa Kizayuni hautaondoka salama kutokana na jinai kubwa waliyoitenda.

Ni hakika kwamba Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vitampiga adui huyu muovu kwa nguvu. Wananchi wa Iran wako nasi, wanalisaidia jeshi, na Jamhuri ya Kiislamu, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, litapata ushindi dhidi ya utawala wa Kizayuni. Taifa letu tukufu litambue hili, liwe na yakini, na lijue kwa hakika kuwa kila juhudi itaelekezwa katika kufanikisha lengo hilo.

Amani, rehema, na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu nyote.

Chanzo: Khamenei.ir

captcha