IQNA

Russia yasisitiza kuwa Ukraine lazima ipokonywe silaha

23:25 - March 03, 2022
Habari ID: 3475002
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema, nchi yake inataka iwepo orodha ya silaha ambazo Ukraine haitaweza katu kuwa na nazo na wala hazitatengenezwa nchini humo.

Sergey Lavrov amesisitiza kwa mara nyingine tena kuhusu ulazima wa Ukraine kupokonywa silaha na akasema, inapasa wananchi wa Ukraine waamue kuhusu mustakabali wao.

Halikadhalika, Lavrov amekanusha kama Russia ina nia ya kuihodhi Ukraine na akasisitiza kwamba, nchi yake iko tayari kwa mapatano ya kufikia njia ya ufumbuzi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza kuwa, kuna uhakika mwingi wa mambo unaothibitisha kuwa Ukraine ni sehemu ya mpango wa Magharibi wa kuanzisha "ukanda wa kiuadui" wa kuizunguka Russia na kwamba, kwa muda wa miaka miwili sasa, nchi hiyo imekuwa ikisheheneshwa silaha, ambapo katika miezi ya karibuni shehena za zana za kijeshi zimeongezeka nchini humo kwa kiwango kikubwa.

Lavrov amevilaumu pia vyombo vya habari na wanasiasa wa nchi za Magharibi kwa kufumbia macho matatizo na mateso ya watu wa eneo la Donbas, ambao amesema "wameshambuliwa na kuuawa kwa makombora kwa muda wa miaka minane" na akaongeza kuwa, lengo jengine kuu inalofuatilia Russia huko Ukraine ni "kuondoa uajinabia".

Kwingineko, Jeshi la Russia limetangaza kuwa limeuteka mji wa Bahari Nyeusi wa Kherson wa nchini Ukraine huku likiendelea kusonga mbele katika miji mingine ya nchi hiyo ya Ulaya Mashariki.

Gennady Lakhuta, meya wa mji huo amethibitisha habari hiyo huku shirika la habari la Reuters likisema kuwa wanajeshi wa Russia wako katika kila kona ya mji huo wa Kherson.

Meya Igor Kolykhaiev amesema kuwa mazungumzo yanaendelea kati yao na wanajeshi wa Russia waliongia kwenye mji huo.

Amesema, sisi hapa hatuna silaha zozote na wala hatuna uadui. Tumeonesha kivitendo kuwa lengo letu ni kuhakikisha mji hauharibiwi na tunajaribu kukubaliana na hali ya uvamizi na kuepusha kutokea mauaji.

Vile vile ameandika katika mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba: Hivi sasa tuna kibarua kizito cha kukusanya na kuzika watu waliokufa pamoja na kugawa chakula na madawa, kukusanya taka, kudhibiti hali ya usalama n.k.

Ikumbukwe kuwa, baada ya viongozi wa maeneo yaliyojitangazia uhuru ya Donetsk na Luhansk mashariki ya Ukraine kuiomba Russia iwatumie misaada ya kijeshi kulingana na mikataba ya ushirikiano iliyoko baina yao, siku ya Alkhamisi ya tarehe 24 Februari, Rais Vladimir Putin wa Russia alitangaza kuanza operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbas ziliko jamhuri hizo mbili zilizojitenga na Ukraine.

Mara kwa mara Russia imekuwa ikisema kuwa, lengo lake si kukalia kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo, bali ni kuipokonya silaha ili kulinda usalama wake wa kitaifa kutokana na kuwa Ukraine imekuwa ikijikurubisha na shirika la kijeshi la NATO linaloongozwa na Marekani.

4040106/

Kishikizo: russia ukraine
captcha