Aiman Ridhwan Mohamad Ramlan ameshinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha tilawa katika Mashindano ya 65 ya Kimataifa y Usomaji na Kuhifadhi Qur’ani Tukufu (MTHQA) yaliyofanyika Kuala Lumpur. Hii ilikuwa mara yake ya pili kushiriki mashindano haya, baada ya kuwakilisha Malaysia mwaka 2022.
Kijana huyu mwenye umri wa miaka 27 kutoka Taiping, Perak, alisema ushindi huu ndio kilele cha safari yake ya tilawa. “Alhamdulillah, ninahisi furaha na msisimko mkubwa kwani hii ndiyo mara yangu ya kwanza kushinda ubingwa wa kimataifa,” aliwaambia waandishi wa habari wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi, kwa mujibu wa taarifa ya Bernama.
Aiman, ambaye alianza kushiriki mashindano ya tilawa akiwa na umri wa miaka 15, alisema amejifunza kutoka kwa mabingwa wa Malaysia na pia kuanzisha urafiki na maqari kutoka nchi kama vile Iran na Indonesia.
Mabadilishano hayo, amesema, yalimsaidia sana kuongeza uelewa wake wa taranum na kuboresha ufasaha wa sauti yake. Pia alisisitiza umuhimu wa maandalizi yake katika tajweed, utamkaji sahihi, ubora wa sauti na ladha ya qiraa’ah yenye lahja nzuri.
Mapema mwaka huu, katika mwezi wa Ramadhani, Aiman alionekana katika kipindi cha Mahfel TV cha Iran. Alitoa tilawa iliyochanganya ladha ya Misri na ladha ya Malaysia, kisha akaimba nasheed kumhusu Mtume Muhammad (SAW). Katika mahojiano hayo, pia alizungumzia utamaduni wa Qur’ani nchini Malaysia ndani ya jamii yao yenye makabila na tamaduni mchanganyiko.
Katika kipengele cha wanawake, Wan Sofea Aini Wan Mohd Zahidi kutoka Kelantan alitwaa taji la qariah licha ya kuugua kabla tu ya mashindano.
Alisema msaada wa familia, walimu na marafiki ulimpa moyo wa kuendelea. Siku mbili kabla ya mashindano, alipata mafua yaliyosababisha sauti yake kuwa na ukakasi, lakini aliweza kukamilisha tilawa bila matatizo makubwa.
Washindi wa mashindano ya tilawa na ya hifdhi kila mmoja alipokea zawadi ya fedha taslimu ya RM40,000, vito kutoka Yayasan Pembangunan Ekonomi Islam Malaysia (YaPEIM), zawadi nyingine, na vyeti vya shukrani.
Mwaka huu, mashindano hayo yaliyofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 9 chini ya kaulimbiu “Kuendeleza Ummah wa MADANI” yalileta pamoja washiriki 71 kutoka nchi 49.
/3494183/