IQNA

Bunge la Morocco lajadili uendelezaji wa Mafunzo ya Kuhifadhi Qur’ani Tukufu

15:37 - December 05, 2025
Habari ID: 3481615
IQNA – Bunge la Morocco limefanya kikao maalumu kujadili hali ya taasisi na vituo vya Qur’ani vilivyobobea nchini humo katika kuendeleza elimu ya wahifadhi wa Qur’ani Tukufu.

Kikao hicho kilifanyika Jumatatu na kushuhudia mjadala mpana kuhusu maendeleo ya mifumo ya kidini kwa vituo vya Qur’ani na nafasi ya taasisi maalumu, hususan Kituo cha Mohammed VI cha Tilawa na Masomo ya Qur’ani, katika kuinua ubora wa elimu ya wahifadhi wa Qur’ani.

Mjadala huo ulijitokeza baada ya wabunge kadhaa kuuliza Wizara ya Awqaf na Masuala ya Kiislamu kuhusu maendeleo ya elimu katika uwanja huu, wakisisitiza kuwa uwezo wa kuhifadhi Qur’ani ni nguzo kuu ya kulinda utambulisho wa kidini wa Morocco.

Katika kujibu maswali ya wabunge kuhusu mafanikio ya Kituo cha Qur’ani cha Mohammed VI, Waziri wa Awqaf Ahmed El-Tawfiq alisema kuwa kwa juhudi na kozi za mafunzo ya kina, Morocco sasa ina idadi kubwa ya wahifadhi wa Qur’ani wenye uwezo na umahiri.

Akaongeza kuwa kituo hicho kina wahifadhi wengi waliobobea katika Qira’at mbalimbali (mitindo ya usomaji wa Qur’ani). El-Tawfiq alibainisha kuwa kituo hicho kimekuwa nguzo muhimu katika kulea kizazi kipya cha wahifadhi wa Qur’ani kwa viwango vya juu, huku shughuli zake zikitegemea utaalamu wa kielimu na kufuata taratibu za kitaalamu.

Aidha, alikumbusha kuwa mwaka 2024, Kituo cha Mohammed VI kilichaguliwa na kuheshimiwa kama taasisi bora zaidi ya Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu na waandaaji wa Tuzo ya Qur’ani ya Kuwait.

Morocco, nchi ya Kiarabu Kaskazini mwa Afrika inayopakana na Bahari ya Atlantiki na Mediterania, inajulikana kwa wingi wa Waislamu wake, ambapo takribani asilimia 99 ya wananchi wanashikamana na dini ya Kiislamu.

/3495610

Kishikizo: qurani tukufu morocco
captcha