IQNA

Wasiwasi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mapigano ya kidini nchini Ethiopia

12:03 - May 09, 2022
Habari ID: 3475226
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amebainisha masikitiko yake juu ya mapigano makali ya hivi karibuni kati ya Waislamu na Wakristo wa Orthodox nchini Ethiopia, ambapo takriban watu 30 waliripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa.

"Ninatoa wito kwa mamlaka ya Ethiopia kuanzisha uchunguzi wa haraka na wa kina, huru na wa uwazi katika kila moja ya matukio haya mabaya na kuhakikisha kwamba wale watakaobainika kuhusika wanachukuliwa hatua," Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet amesema katika taarifa yake.

Amesema mapigano hayo ya kidini yaliripotiwa kwa mara ya kwanza huko Gondar, mji ulioko kaskazini mwa mkoa wa Amhara, Aprili 26, ambayo yaliripotiwa kuhusishwa na mzozo wa ardhi, na kuenea haraka katika miji midogo na mikubwa katika mikoa mingine mingi na mji mkuu,  Addis Ababa.

Ameongeza, "Ninaelewa misikiti miwili imechomwa moto na mingine miwili imeharibiwa kidogo huko Gondar.

"Katika mashambulizi ya dhahiri ya kulipiza kisasi yaliyofuata, wanaume wawili Wakristo wa Orthodox waliripotiwa kuteketezwa hadi kufa, mtu mwingine alikatwakatwa hadi kufa, na makanisa matano kuteketezwa katika eneo la Silt'e…. lililoko kusini-magharibi mwa nchi.”

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kulikuwa na ghasia zaidi tarehe 28 Aprili katika mji wa Debark katika eneo la Amhara, na katika mji wa Dire Dawa kaskazini mashariki mwa eneo la Afar.

Polisi wameripotiwa kuwashikilia takriban watu 578 katika takriban miji minne iliyohusishwa na mapigano hayo makali.

"Uwajibikaji wa mtu binafsi kwa wahalifu ni muhimu ili kuzuia ghasia zaidi," amesema Bachelet.

Bachelet amesisitiza kuwa sababu za msingi za vurugu hizi za kushtua lazima zishughulikiwe haraka "kwa ushiriki wa maana wa waathirika, familia na jumuiya zilizoathirika" ili kuzuia ghasia zaidi kati ya dini.

Wakristo wa Orthodox ni takribani  asilimia 43 ya watu milioni 120 wa Ethiopia, wakati zaidi ya theluthi moja ni Waislamu.

4055408

Kishikizo: ethiopia ، wakristo ، waislamu
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :