IQNA

Awamu ya Awali ya Kusoma Qur’ani Tukufu Yaanza Rasmi Nchini Qatar

14:14 - November 10, 2025
Habari ID: 3481494
IQNA – Awamu ya kwanza ya mashindano ya Qur’ani Tukufu ya Sheikh Jassim bin Muhammad bin Thani imeanza rasmi nchini Qatar, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Awqaf na Mambo ya Kiislamu.

Wizara hiyo imetangaza kuwa mitihani ya awali inaendelea kwa wanaume na wanawake wakazi wa Qatar, katika mashindano ya kuhifadhi Qur’ani kwa kiwango cha sehemu na cha jumla, ikiwa ni sehemu ya mashindano ya 30 ya Sheikh Jassim bin Muhammad bin Thani yanayoandaliwa na wizara hiyo.

Fahad Ahmed Al Mohammed, ambaye ni mjumbe wa kamati ya maandalizi, ameeleza kuwa washiriki wa jinsia zote wanachuana katika moja ya fani tukufu zaidi za elimu ya Kiislamu. Washiriki 15 kutoka kila kundi, yaani wahifadhi wa Qur’ani kwa jumla na kwa sehemu, watachaguliwa kuingia awamu ya pili.

Mashindano haya yanajitofautisha kwa kuhimiza washiriki kusoma kwa mitindo mbalimbali ya kisomo cha Qur’ani (qira’at), na kuhifadhi maarifa haya kwa moyo, jambo ambalo halipatikani kwa urahisi katika mashindano ya kimataifa. Al Mohammed amesisitiza kuwa washindi wa kuhifadhi kwa jumla katika riwaya moja hulazimika kushiriki kwa riwaya tofauti katika mashindano yajayo, hali inayochochea kujifunza riwaya nyingi na kueneza elimu hii adhimu ya Qur’ani.

Kwa mwaka huu, jumla ya washiriki 68 wa jinsia zote wanachuana katika riwaya 13 tofauti, huku awamu ya kwanza ikiwajumuisha washiriki 1,493 kutoka mataifa 57. Kati yao, 731 wamehifadhi sehemu ya Qur’ani na 384 wamehifadhi kwa jumla. Idadi ya wanawake waliojiandikisha ni 79 katika kundi la wahifadhi wa jumla na 299 katika kundi la kuhifadhi kwa sehemu.

Usimamizi wa mitihani unafanywa na kamati 11 kwa washiriki wa kiume, kila moja ikiwa na Mwenyekiti, Mjumbe wa Kamati, na Mwakilishi kutoka Kamati ya Maandalizi. Kwa upande wa wanawake, kuna kamati 8 za majaji kwa makundi yote mawili.

Mitihani ya awamu ya kwanza itaendelea hadi tarehe 12 Novemba. Washiriki wa kiume wanapimwa katika Msikiti wa Imam Muhammad bin Abdul Wahab katika vipindi vya asubuhi na jioni. Kipindi cha asubuhi huanza saa 1:30 alfajiri, na cha jioni huanza saa 9:00 alasiri. Washiriki wa kike wanapimwa katika Kituo cha Shughuli za Wanawake kilichopo eneo la Al Waab, katika kipindi cha jioni kinachoanza saa 8:30 alasiri.

3495319

captcha