IQNA

Maonyesho ya 29 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran yazinduliwa

17:51 - April 17, 2022
Habari ID: 3475133
TEHRAN (IQNA)- Maonyesho ya 29 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Tehran yamefunguliwa Jumamosi jioni katika sherehe iliyohudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu serikalini.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, sherehe za kufungua maonyesho hayo zimehudhuriwa na Spika wa Bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf, Waziri wa Utamaduni na Muongozi wa Kiislamu Mohammad Mehdi Esmaeili, na Waziri wa Elimi Yousef Nouri miongoni mwa wengine.

Maonyesho hayo ambayo yanafanyika katika Ukumbi wa Sala (Musalla) wa Imam Khomeini mjini Tehran yalianza kwa qiraa ya Qur'ani Tukufu ya qarii wa kimataifa wa Iran Hadi Movahid Amin.

Waziri wa Utamaduni Esmaeili alikuwa mzungumzaji wa kwanza aliyetoa maelezo kuhusu maonyesho hayo.

Akiashiria ulazima wa kufanyika matukio hayo ana kwa ana baada ya janga la corona, amesema: "Jamii yetu ina haja kubwa ya mikusanyiko hii ya Qur'ani na kufungwa kwa matukio haya kuna athari isiyonzuri kwa watu."

Alibainisha kuwa mwanzoni takribani mita za mraba 18,000 zilitengwa kwa ajili ya maonyesho hayo lakini kutokana na mapokezi makubwa ya mashirika na taasisi mbalimbali, jumla ya eneo la maonyesho lilipanuliwa na kufikia mita za mraba 40,000.

Qalibaf pia alihutubia sherehe hiyo, akisikitika kwamba watu hawakuweza kutumia maonyesho haya katika miaka miwili iliyopita kutokana na janga la corona.

Akiuelezea mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni fursa adhimu, alitumai kwamba waja wangeweza kuelewa kikweli Quran na usiku wa Qadr.

Katika sehemu nyingine amesema Mapinduzi ya Kiislamu yamepinga maadui kutokana na imani na maadili ya Qur'ani.

Maonyesho hayo yataendeshwa kwa muda wa wiki mbili, yakikaribisha wageni kila siku kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa sita usiku.

Kwa kauli mbiu ya "Quran, Kitabu cha Matumaini na Utulivu", maonyesho hayo yatafanyika yakiwa na sehemu 45 zikiwa zimejengwa katika eneo la mita za mraba 40,000.

Maonesho ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran kila mwaka huandaliwa na Wizara ya Utamaduni na Muongozo ya Kiislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Maonyesho hayo yanalenga kukuza dhana za Qur'ani na kuendeleza shughuli za Qur'ani.

Aidha yanaonyesha mafanikio ya hivi punde zaidi ya Qur'ani nchini humo na pia bidhaa mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kutangaza Kitabu hicho Kitakatifu.

captcha