IQNA

Mjumuiko kijijini Misri kuwatunuku wahifadhi wa Qur’ani

15:30 - December 16, 2025
Habari ID: 3481667
IQNA – Shule ya kuhifadhi Qur’ani ya “Ibad al-Rahman” iliyopo kijiji cha Atu, karibu na mji wa Bani Mazar katika mkoa wa Minya kaskazini mwa Misri, iliandaa mjumuiko maalumu kwa ajili ya kuwasherehekea wahifadhi wa Qur’ani wa kijiji hicho.

Mamia ya wakazi wa kijiji walijitokeza, wakiambatana na masheikh na wanazuoni wa Al-Azhar, wawakilishi wa Wizara ya Awqaf, walimu wa kuhifadhi Qur’ani, pamoja na walimu wa kike wa Qur’ani kutoka kijijini humo, kama ilivyoripoti tovuti ya Ad-Dustur.

Wakati wa maandamano, wahifadhi hao walibeba nakala za Qur’ani Tukufu kama njia ya kuhamasisha wengine kuifuata njia ya kuhifadhi Kitabu Kitukufu.

Zawadi zilitolewa kwa wanafunzi wa kiume na wa kike, kuanzia shule za msingi hadi sekondari, waliokamilisha kuhifadhi Qur’ani.

Miongoni mwa wahifadhi walikuwemo watoto wadogo wenye umri wa miaka 10.

Waandaaji waliwapatia vyeti vya pongezi pamoja na zawadi za fedha, kulingana na kiwango cha hifdhi walichofikia.

Hafla hiyo pia ilimuenzi mwanafunzi Hala Khalil Ibrahim, ambaye ana ulemavu wa mwili. Pamoja na changamoto zake, aliendelea kusoma na kuhifadhi Qur’ani akiwa mwanafunzi wa shule ya Qur’ani ya kijiji.

Hala alijikuta akitokwa na machozi alipoitwa jukwaani kupokea tuzo yake. Tukio hilo liliwagusa sana waliokuwepo, na wakamkimbilia kwa upole, wakambeba kwa kiti cha magurudumu hadi jukwaani.

Sherehe hiyo ilihitimishwa kwa kuwatuza pia masheikh waliowafundisha wanafunzi, pamoja na kumtambua mkuu wa shule hiyo, Sheikh Rabi’ Nahas, na msimamizi wake, Sheikh Ahmed Mohammed Fahmy.

3495754

captcha