IQNA

Al-Azhar yakaribia kukamilisha mradi wake maalum wa hati ya Qur'ani

21:11 - February 18, 2025
Habari ID: 3480235
IQNA – Al-Azhar ya Misri inakaribia hatua za mwisho za mradi wake wa kipekee wa hati ya Qur'ani, huku sehemu kubwa ya kazi ikiwa imekamilika, kulingana na Mohamed Al-Duwaini, Naibu wa Al-Azhar.

Akizungumza kwenye hafla ya Kiarabu katika Msikiti Mkuu wa Al-Azhar, Al-Duwaini alitangaza kwamba mashindano ya kitaifa yalifanyika ili kuchagua waandishi bora wa kaligrafia na wachoraji wa mapambo wa Misri kwa ajili ya mradi huo.

“Waandishi watatu wa kaligrafia na wachoraji sita wa mapambo waliingia hatua ya mwisho, ambapo kila mwandishi wa kaligrafia aliandika Juzuu' moja kamili ya Qur'ani,” alisema.

Baada ya tathmini kufanywa na kamati ya maprofesa wa kaligrafia, heshima ya kukamilisha hati hiyo ilitunukiwa Mwalimu wa Kaligrafia Mahmoud Al-Sahli. Al-Duwaini alibainisha kuwa, “Kwa kukamilika kwa mradi huu, Al-Azhar itakuwa na Qur'ani yake ya kipekee.”

Kongamano hilo lilijumuisha maonyesho maalum yaliyoonyesha kazi za washiriki wa mwisho wa mashindano na lilihusisha pia warsha na majadiliano kuhusu historia ya uandishi wa Qur'ani.

Akisisitiza umuhimu wa kitamaduni wa sanaa katika Uislamu, Al-Duwaini alisema, “Sanaa ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Kiislamu. Waislamu wamepata umahiri si tu katika fasihi kama vile ushairi na insha, bali pia katika usanifu majengo, kaligrafia, mapambo ya Qur'ani, na upambaji wa Kiarabu.”

Aliongeza kuwa kaligrafia imekuwa kiini cha elimu ya Kiislamu, akisema, “Kupitia uandishi wa uangalifu na mapambo ya Qur'ani, Waislamu wamehifadhi maandiko yao matakatifu. Kaligrafia pia ilichangia pakubwa katika utayarishaji wa hati za kielimu zilizotungwa na wanazuoni.”

Kongamano la Tatu la Kaligrafia ya Kiarabu na Mapambo, lilioandaliwa chini ya usimamizi wa Imamu Mkuu Ahmed Al-Tayeb, lilianza Februari 17 katika Msikiti Mkuu wa Al-Azhar. Hafla hiyo, iliyohudhuriwa na wanazuoni wa Al-Azhar na wasanii maarufu, itaendelea hadi Februari 25.

3491898

Kishikizo: qurani tukufu misri
captcha