IQNA

Roboti inayoendeshwa na Akili Mnemba kuwasaidia Mahujaji Saudia

19:07 - May 23, 2025
Habari ID: 3480727
IQNA –Roboti mpya ya Manarat Al-Haramain inayotumia Akili Mnemba (AI) imezinduliwa ili kuwasaidia Mahujaji huko Makka, Saudi Arabia.

Kadri maandalizi yanavyoendelea nchini Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija, Mahujaji wanaohitaji msaada mwaka huu wataweza kutumia huduma za msaidizi mpya wa kisasa anayeunganisha mila za Uislamu na maendeleo ya hivi karibuni katika teknolojia ya Akili Mnemba. 

Uongozi wa Masuala ya Kidini katika Msikiti Mkuu wa Makka na Msikiti wa Mtume umezindua toleo la pili lililoboreshwa la roboti ya Manarat Al-Haramain siku ya Jumatano, ikiwa ni sehemu ya mpango unaolenga kutumia teknolojia za hali ya juu ili kuboresha uzoefu wa kiroho wa Mahujaji. 

Ilielezwa kuwa roboti hiyo itakuwa kituo cha marejeleo kwa maswali ya kidini katika Msikiti Mkuu na itaweza kuwaunganisha waumini na wageni wengine na mufti kwa simu za video moja kwa moja ili kujibu maswali yao. 

Toleo jipya la roboti hiyo inapatikana katika Misikiti Miwili Mitakatifu ya Makka, Masjid Al Haram na Msikiti wa Mtume, Al Masjid An Nabawi jijini Madina. Inachanganya uhalisia, usasa na teknolojia ya hali ya juu ili kuboresha uzoefu wa Mahujaji kwa kuwapatia njia rahisi za kupata taarifa, uongozi wa masuala ya kidini ulisema. 

Ibada ya kila mwaka ya Hija ambayo kila Muislamu anapaswa kuitekeleza angalau mara moja maishani ikiwa ana uwezo wa kimwili na kifedha, inatarajiwa kuanza Makka tarehe 4 Juni na kukamilika tarehe 9 Juni. 

Mahujaji kutoka kote duniani wameanza kuwasili Saudi Arabia mwezi huu.

3493190

Kishikizo: roboti hija akili
captcha