IQNA

Al-Azhar yaonya kuhusu magaidi wa Daesh kutumia Akili Mnemba kuvutia wafuasi

12:38 - December 01, 2025
Habari ID: 3481599
IQNA – Kituo cha Al-Azhar cha Kupambana na Mielekeo ya Ugaidi kimeeleza wasiwasi wake kuhusu matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) kwa madhumuni ya kuajiri wafuasi wapya.

Kituo hicho kimeonya kuwa hatua hiyo inaongeza changamoto kwa wale wanaojitahidi kupambana na misimamo mikali.

Hivi karibuni, gazeti la Uingereza Daily Telegraph lilifichua kuwa magaidi wa ISIS  (Daesh)  kwa mara ya kwanza limetumia teknolojia ya Akili Mnemba kama chombo cha uajiri nchini Uingereza, jambo lililozua hofu kubwa miongoni mwa mashirika ya ujasusi ya taifa hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idara ya usalama wa ndani ya Uingereza (MI5) na idara ya ujasusi wa kimataifa (MI6) zinachunguza kwa makini namna Daesh inavyotumia Akili Mnemba kusambaza propaganda na kuendesha shughuli za kuwavutia vijana wajunge na kundi hilo la kigaidi.

Hayo yanajiri huku kukiwa na hofu kwamba Daesh na al-Qaeda wanajipatia tena nguvu katika Asia ya Magharibi na Pembe ya Afrika.

Kituo cha Al-Azhar kimeeleza wasiwasi wake juu ya ripoti hiyo, kikisema kuwa Daesh imeanza kutumia teknolojia ya Akili Mnemba kwa mara ya kwanza kuvutia wanachama wapya nchini Uingereza na kuchochea mashambulizi, sambamba na wito wa kujiunga na maeneo ya vita nchini Syria.

Kituo hicho kimesisitiza kuwa maendeleo haya ni mgeuko hatari katika mbinu za kidijitali za propaganda za makundi ya kigaidi, na yanaonyesha juhudi zao za kuendeleza matumizi ya teknolojia ili kupanua uwezo wao wa uharibifu.

Aidha, Kituo cha Al-Azhar kimeongeza kuwa uwezo wa makundi ya kigaidi kutumia Akili Mnemba kutafsiri kwa wakati mmoja katika lugha kadhaa na kusambaza maudhui ya propaganda kwa kasi isiyo na kifani,  wakirudia simulizi zao kwenye mitandao ya kijamii kabla hazijagunduliwa na kuondolewa, ni mabadiliko makubwa katika zana za uajiri na unaongeza changamoto kwa wanaopambana na misimamo mikali na kusimamia maudhui mtandaoni.

Kituo hicho kimetaka mashirika ya kimataifa kushirikiana zaidi katika kufuatilia maudhui ya kigaidi ya kidijitali, kutekeleza udhibiti wa kiufundi wa hali ya juu kwenye majukwaa ya wazi, na kuimarisha zana za kupinga Akili Mnemba zinazoweza kugundua mifumo ya propaganda kabla haijachapishwa.

Kituo cha Al-Azhar kimehitimisha kwa kukumbusha kuwa toleo la 13 la jarida lake “A Step Forward” lilihusisha makala inayozungumzia Akili Mnemba, uhusiano wake na misimamo mikali, matumizi yake na makundi ya kigaidi, athari zake kwa maadili ya kijamii, na namna Akili Mnemba inaweza kutumika kupambana na misimamo mikali.

Makala hiyo inapatikana katika sehemu ya machapisho ya kituo hicho kwenye tovuti ya kielektroniki ya Al-Azhar.

Daily Telegraph pia imeripoti kuwa, mbali na kuchochea mashambulizi barani Ulaya, Daesh imezindua kampeni mpya ya kuajiri wapiganaji wa kigeni kwenda Syria. Wakati wa kilele cha nguvu za Daesh, zaidi ya wapiganaji wa kigeni 30,000, wakiwemo raia 900 wa Uingereza,  walielekea Asia ya Magharibi kujiunga na kundi hilo la kigaidi. Wengi waliuawa, na idadi kubwa ya waliorejea walifunguliwa mashtaka.

Kuna hofu kwamba kizazi kipya cha vijana Waingereza kinajiriwa na Daesh kupitia teknolojia mpya na mitandao ya kijamii. Wiki iliyopita, kijana mwenye umri wa miaka 18 kutoka kusini mwa London alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Gatwick alipokuwa akijaribu kupanda ndege kuelekea Istanbul, na akashtakiwa kwa kupanga kujiunga na Daesh nchini Syria.

Daily Telegraph inaripoti kuwa shughuli za Daesh nchini Syria zimeongezeka katika miezi ya hivi karibuni, huku vitengo vidogo vya kundi hilo vikifanya mashambulizi ya msituni dhidi ya vikosi vya serikali na “SDF.”

Wakati huohuo, Daesh inatumia teknolojia ya Akili Mnemba sambamba na mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe wake kwa hadhira ya kimataifa kwa kasi isiyo na kifani. Kwa msaada wa Akili Mnemba, nyaraka na maudhui ya Kiarabu ,  ikiwemo tahariri za kila wiki za Daesh,  hutafsiriwa katika lugha kadhaa na kisha kuchapishwa kwenye majukwaa kama Facebook, yakifikia hadhira kubwa kabla ya kufutwa.

4319813

Habari zinazohusiana
captcha