IQNA

Mtazamo

Saumu husaidia Kuboresha Umakini, Kuimarisha Kumbukumbu

16:38 - March 06, 2025
Habari ID: 3480315
IQNA – Kufunga husaidia kuongeza umakini kwa kuleta mpangilio katika maisha ya kila siku na kupunguza usumbufu unaotokana na ulaji na unywaji mfululizo.

Wakati mtu anapojizuia kula na kunywa, anaweza kuelekeza nishati yake ya kiakili zaidi kwenye masuala ya kiroho na shughuli za kielimu.

Mbali na vipengele vyake vya kiroho, kufunga kuna athari kubwa za kimwili na kisaikolojia. Moja ya athari hizi ni kuongezeka kwa umakini na kuboreshwa kwa kumbukumbu, ambazo hutokana na michakato ya kimwili na kiakili inayohusiana na kufunga.

Wakati mtu anapojizuia kula na kunywa, anaweza kuelekeza nishati yake ya kiakili zaidi kwenye masuala ya kiroho na shughuli za kielimu. Hali hii inaweza kuonekana sana hasa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao ni kipindi cha ibada nyingi na usomaji wa Qur'an kwa wale wanaofunga.

Qur'ani Tukufu inasema katika Aya ya 45 ya Surah Al-Ankabut:

Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda.."

Ingawa aya hii inazungumzia sala moja kwa moja, tafsiri pana inaonyesha kuwa ibada yoyote, ikiwemo kufunga, inaweza kuisafisha akili dhidi ya mawazo mabaya na kuiweka kwenye kumkumbuka Mungu, jambo ambalo huongeza umakini.

Kufunga huimarisha kumbukumbu kwa kuleta mabadiliko chanya mwilini, kama vile kupunguza viwango vya sukari kwenye damu na kuongeza uzalishaji wa protini za ubongo.

Kufunga kunaweza kuongeza idadi ya neva za ubongo na kuboresha utendaji wa kiakili. Katika miaka ya hivi karibuni wataalamu wengi wa afya wasiokuwa Waislamu wamekuwa wakishauri watu kufunga kwa muda yaani kujizuia kula mlo moja au miwili (intermittent fasting).

Wataalamu wamebaini kuwa Kufunga kwa muda wa kati kumesaidia kuimarisha utendaji wa ubongo. Kwa kuongeza uwezo wa mwili kuzalisha protini inayoitwa BDNF, kufunga kwa muda wa kati husaidia kuboresha kumbukumbu, uwezo wa kujifunza na kazi nyingine za kiutambuzi.

Kwa ujumla, kufunga husaidia kuboresha umakini na kuimarisha kumbukumbu kwa kuleta usawa kati ya mwili na akili. Hii inafanikishwa kwa kukuza nidhamu ya kibinafsi, kupunguza usumbufu wa kimwili, na kuongeza umakini kwa masuala ya kiroho.

Qur'ani Tukufu pia inasisitiza umuhimu wa kujidhibiti na kumkumbuka Mungu, ikieleza kwa njia isiyo ya moja kwa moja athari chanya za kufunga.

Kwa kufunga wakati wa Ramadhani, mtu hawezi tu kupata afya ya kimwili, bali pia anaweza kuboresha utendaji wake wa kiakili na kisaikolojia.

Mwezi huu unatoa fursa ya kusafisha akili, kuongeza umakini, na kuimarisha kumbukumbu kupitia ibada na kujiboresha binafsi.

3492194

captcha