IQNA

Imam Khamenei amjibu Trump: Meli za kivita zinaweza kuzamishwa baharini

16:32 - February 17, 2026
Habari ID: 3481951
IQNA-Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu vitisho vya mara kwa mara vya kijeshi kutoka Marekani dhidi ya Iran, akisema kuwa silaha zenye uwezo wa kuzamisha manowari za Marekani ni “hatari zaidi” kuliko meli hizo za kivita zenyewe.

Akizungumza Jumanne jijini Tehran alipohutubia maelfu ya wananchi kutoka Mkoa wa Azarbaijan Mashariki, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesema:

“Rais wa Marekani [Donald Trump] mara kwa mara anadai kuwa jeshi lao ndilo lenye nguvu zaidi duniani. Hata hivyo, hata jeshi linalodaiwa kuwa na nguvu zaidi linaweza kupigwa kwa namna ambayo haliwezi tena kusimama.”

Ameongeza kuwa: “Wanasema mara kwa mara kwamba, ‘Tumetuma manowari kuelekea Iran.’ Sawa—bila shaka manowari inayobeba ndege za kivita ni kifaa hatari. Lakini kilicho hatari zaidi kuliko manowari hiyo ni silaha yenye uwezo wa kuizamisha hadi chini ya bahari.”

Ayatullah Khamenei pia ameashiria kauli za Trump kwamba Washington haijaweza kuupindua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kipindi cha miaka 47, akisema kuwa hilo ni kukiri kufeli kwa njama hizo. Amesema:

“Kwa miaka 47, Marekani imeshindwa kuangamiza Jamhuri ya Kiislamu,” kisha akamhutubu Trump na kuongeza: “Ninasema wazi: hamtaweza kufanya hivyo hata siku zijazo.”

Onyo hilo linakuja wakati Rais wa Marekani, Donald Trump, akiendelea kupeleka vikosi vya kijeshi katika eneo la Asia Magharibi karibu na Iran, huku akitishia mashambulizi dhidi ya nchi hiyo.

Maafisa wa Marekani walisema tarehe 12 Februari kwamba Wizara ya Vita (Pentagon) ilikuwa inatuma manowari nyingine ya kubeba ndege katika eneo hilo, pamoja na maelfu ya wanajeshi, ndege za kivita, na meli za kivita zenye makombora.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameashiria pia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kati ya Tehran na Washington.

Amesema: “Kauli hizi anazotoa rais wa Marekani, wakati mwingine vitisho, wakati mwingine masharti ya nini kifanyike au kisifanyike, zinaonyesha wazi kuwa wanataka kulitawala taifa la Iran.”

Akifafanua ameongeza: “Wanasema, ‘Hebu tujadili nishati yenu ya nyuklia,’ lakini matokeo ya mazungumzo hayo tayari yameamuliwa: kwamba msibaki tena na nishati hiyo. Kuamua matokeo kabla ya mazungumzo hata kuanza ni kosa na ni upumbavu.”

Amesema pia: “Hii ndiyo njia ya kipumbavu inayofuatwa na marais wa Marekani, maseneta fulani, rais wa sasa, na wengine.”

Hata hivyo, Kiongozi Muadhamu amesema: “Wananchi wa Iran wanaifahamu vyema misingi ya Kiislamu na Kishia,” kisha akanukuu kauli ya Imam Hussein (AS) aliyesema:

‘Mtu kama mimi hawezi kamwe kutoa utii kwa mtu kama Yazid.’ Imam Khamenei ameongeza kuwa: “Kwa hakika, taifa la Iran linasema jambo hilo hilo: taifa lenye utamaduni huu, historia hii, na thamani hizi za juu haliwezi kamwe kutoa utii kwa watu wafisadi kama walioko madarakani Marekani leo.”

Silaha za kujilinda

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kuwa ni jambo la msingi na la lazima kwa taifa kumiliki silaha za kuzuia mashambulizi (deterrence), akisema: “Nchi yoyote isiyokuwa na silaha za kujilinda itakanyagwa na maadui zake.

Hata hivyo, Wamarekani huingilia masuala ya kijeshi na kudai kwamba hatupaswi kuwa na aina fulani au masafa fulani ya makombora.

Hili, kwa hakika, ni suala la taifa la Iran na halihusiani nao hata kidogo.” Ametaja pia kuingilia kwa Marekani haki ya Iran ya kunufaika na teknolojia ya nyuklia ya amani, kwa ajili ya kuendesha nchi, pamoja na matumizi ya kitabibu, kilimo, na nishati, kama mfano mwingine wa kutokuwepo kwa mantiki katika msimamo wao. 

Akizungumza moja kwa moja kwa Wamarekani, alisema: “Hili ni jambo linalohusu taifa la Iran. Linawahusu nini nyinyi?” Imam Khamenei amekumbusha kuwa haki ya kumiliki vituo vya nyuklia na kufanya urutubishaji wa urani inatambuliwa kwa nchi zote chini ya mikataba na kanuni za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA). Amesisitiza kuwa kuingilia kwa Marekani haki za kitaifa za wengine ni dalili ya mtazamo usio na mpangilio na usio thabiti wa maafisa wao kwa kipindi cha muda mrefu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelezea mfano wa kushangaza zaidi wa kutokuwa na busara kwa Marekani, kuwa ni namna wanavyotoa mwaliko wa mazungumzo. 

Amesema: “Wanasema, ‘Njooni tuzungumze kuhusu nishati ya nyuklia,’ lakini hitimisho la mazungumzo linapaswa kuwa kwamba nyinyi msipate kabisa nishati ya nyuklia!” 

Habari inayohusiana:

Katika sehemu nyingine, Ayatullah Khamenei amesema taifa linaomboleza baada ya ghasia za hivi karibuni zilizoungwa mkono na tawala za kigeni, ambazo zilisababisha vifo vya maelfu ya watu. Ameongeza: “Tuko katika maombolezo kwa damu iliyomwagika.”

Aliwagawanya waliouawa katika makundi matatu.

Kundi la kwanza ni walinzi wa usalama na afya, wakiwemo polisi, wanachama wa Basij, Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), na wengine, aliowataja kuwa “mashahidi wa daraja ya juu.” Kundi la pili ni raia waliokufa bila hatia wakati wa machafuko.

“Nao pia ni mashahidi,” amesema, akisisitiza kuwa waliuawa katika mazingira ya “fitna ya adui.”

Kundi la tatu ni wale waliopotoshwa na kujiunga na ghasia. Akiwaita “watoto wetu,” amesema baadhi yao walimwandikia wakionyesha majuto, na kwamba mamlaka pia imewatambua waliouawa miongoni mwao kama mashahidi.

Isipokuwa vinara wakuu walioungwa mkono na maadui wa kigeni, Ayatullah Khamenei amesema wengine wote wanastahili kuombewa na kusamehewa.

Ghasia hizo zilianza tarehe 8 na 9 Januari, wakati waandamanaji wenye silaha na magaidi walioungwa mkono na tawala za kigeni walipoteka maandamano ya amani yaliyokuwa yakilalamikia hali ya uchumi.

Vurugu hizo, ambazo zilihamasishwa waziwazi na Marekani na utawala wa Israel, zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali ya umma na binafsi, ikiwemo maduka, taasisi za serikali, huduma za jamii, pamoja na mauaji ya mamia ya raia na maafisa wa usalama.

Mamlaka za Iran zimethibitisha kuwa mashirika ya kijasusi ya Marekani na Israel yalihusika moja kwa moja, yakitoa ufadhili, mafunzo, na msaada wa vyombo vya habari kwa waasi na magaidi waliokuwa mitaani.

Kumbukumbu rasmi za Iran zinaonyesha kuwa watu 3,117 waliuawa katika ghasia hizo, wakiwemo raia 2,427, pamoja na wanajeshi na maafisa wa usalama waliouawa na magaidi.

4335010/

captcha