IQNA

Ayatullah Khamenei: Iran haitalegeza msimamo na itakabiliana na magenge ya wahalifu

10:33 - January 10, 2026
Habari ID: 3481785
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kundi la watu waharibifu Alhamisi usiku mjini Tehran waliharibu mali za umma na za wananchi kwa ajili ya kumfurahisha rais wa Marekani huku akisisitiza kuwa Iran haitalegeza msimamo katika kukabiliana na magenge ya wahalifu.

Akizungumza Ijumaa asubuhi jijini Tehran kwa mnasaba wa mwamako wa 19 Dey wa wananchi Waislamu wa mji wa Qum nchini Iran miaka 48 iliyopita dhidi ya utawala wa kiimla wa Shah, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, iwapo Trump ana uwezo, basi kwanza arekebishe mambo yaliyoharibika katika nchi yake.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na maelfu ya wananchi waumini  wa Qum, Kiongozi Muadhamu amesema katika mwamko huo, utawala fisadi wa Shah Pahlavi na muungaji mkono wake mkuu walipata pigo mbele ya taifa la Iran na kuongeza kuwa: "Leo pia taifa la Iran kwa baraka za Mfumo wa Kiislamu litatoa pigo kwa utawala wenye kiburi wa Marekani."

Amesema mfumo wa Kiislamu, ambao uliingia madarakani kwa jitihada za maelefu ya mashahidi, hautalegeza msimamo na utakabiliana na magenge ya wanaotekeleza uharibifu.

Kiongozi Muadhamu ameashiria matukio ya uharibifu yaliyotokea nchini na kusema: "Kuna watu ambao kazi yao ni uharibifu, na jana jijini Tehran na maeneo mengine, magenge ya wahuni waliharibu majengo ya nchi yao kwa ajili ya kumfurahisha rais wa Marekani."

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa rais huyo wa Marekani anafurahishwa na uharibifu uliotokea Iran katika hali ambayo iwapo angeweza basi kwanza angeshughulikia matatizo yanayoikumba nchi yake. Kiongozi Muadhamu amesema mikono ya rais wa Marekani imejaa damu ya maelfu ya Wairani waliouawa katika vita vya siku 12 vya juni mwaka jana. Amesema Rais wa Marekani mwenyewe alikiri kuwa alitoa amri ya vita hivyo vya kichokozi vilivyoanzishwa na utawala haramu wa Israel huku wakati huo huo akidai kuwa anawaunga mkono wananchi wa Iran.

Kuhusu hatima ya Rais wa Marekani, Kiongozi Muadhamu amesema kwa watawala wa kiimla na wenye kiburi kama vile Nimrud, Firauani, Reza Khan na Mohammad Reza Pahlavi waliangushwa wakiwa katika kilele cha kiburi na hivyo rais wa Marekani atakumbwa na hatima kama hiyo.

Ayatullah Khamenei amemsema Marekani ina hasira na taifa la Iran kwa sababu imeshindwa kupora utajiri adhimu wa nchi hii.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matukio ya Amerika ya Latini na jitihada za Marekani za kupora utajiri wa nchi hizo na kuongeza kuwa, Wamarekani bila kuona aibu yoyote , wanatangaza wazi kuwa wanataka kupora utajiri wa eneo hilo. Alikuwa akishiria tukio la Marekani kuvamia Venezuela na kumteka nyara rais Maduro  wa nchi hiyo na mke wake. Punde baada ya hujuma hiyo rais Trump wa Marekani alitangaza bayana kuwa atapora mafuta ya nchi hiyo.

Kiongozi Muadhamu amesema kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu utajiri wa Iran, ukiwemo utajiri wa mafuta, ulikuwa mikononi mwa madola ya kibeberu, Wazauni na vibaraka wao.  Aidha amekumbusha uhasama usio na kikomo wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: "Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, mfumo wa Kiislamu unapata nguvu kila siku na njama zao za kuganusha mfumo huu zimegonga mwamba kiasi kwamba, kinyume cha matakwa yao,  leo Jamhuri ya Kiislamu inatazamwa duniani kama nchi yenye nguvu na heshima."

4327819

Habari zinazohusiana
captcha