IQNA

Imam Khamenei

Iran haina imani na wanaodai kupambana na magaidi wa Daesh

21:52 - October 22, 2014
Habari ID: 1463061
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina imani kwamba, wale wanaodai kuendesha mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIL) katika eneo wana nia ya dhati juu ya suala hilo.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema Jumatatu alasiri alipokutana na kufanya mazungumzo hapa Tehran na Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq. Ameashiria madai yaliyotolewa kuhusu mapambano dhidi ya Daesh na kusisitiza kama ninavyomnukuu" sisi hatuna imani na hao wote wanaotamka maneno hayo kama wana nia ya kweli, na tunaamini kuwa suala la Daesh na ugaidi yanapasa kutafutiwa ufumbuzi na nchi za eneo," mwisho wa kunukuu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa usalama, ustawi, nguvu na izza ya Iraq ikiwa ni muhimu katika eneo, yote hayo yana umuhimu mkubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutangaza uungaji mkono thabiti wa Iran kwa serikali mpya ya Iraq. Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa hali ya sasa ya eneo na ya nchini Iraq ni matokeo ya siasa zisizo za uwajibikaji za madola ya kigeni na baadhi ya nchi za eneo huko Syria. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba wananchi na serikali ya Iraq na khususan vijana wa nchi hiyo wana uwezo mkubwa wa kupambana na magaidi nchini humo na kurejesha amani na kwamba hakuna haja ya kuwepo maajinabi na madola ya kigeni.

Katika mazungumzo hayo, Haidar al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq ameshukuru misaada ya Iran katika mapambano dhidi ya Daesh na kueleza kuwa magaidi watasambaratishwa kwa uono mpana wa mataifa mawili ya Iran na Iraq, uungaji mkono wa maulamaa na kwa miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.../mh

1462696

captcha