IQNA

Mwislamu Ufaransa ahatarisha maisha kuwaokoa Mayahudi

17:23 - January 13, 2015
Habari ID: 2706293
Kijana wa Mwislamu anayejulikana kwa jina la Lassan Bathily amekuwa shujaa nchini Ufaransa baada ya kuwaokoa wanunuzi Mayahudi wakati watu wenye silaha walipolivamia jengo la biashara ya Hyper Cacher mjini Paris siku chache zilizopita.

Lassana Bathily, ameiambia televisheni ya Ufaransa ya BFM kwamba, wakati wanunuzi hao walipokimbilia chini ya jengo hilo, alifungua mlango wa jokofu baada ya kulizima na kuwaficha ndani halafu akazima taa na kuwataka watulie tuli ili aweze kutoka tena nje na kuangalia hali ilivyo.

Watu mbalimbali wamewasiliana kupitia mitandao ya habari wakimwita kijana huyo wa Kiislamu kuwa ni shujaa na kutaka habari yake ienezwe kote ulimwenguni.

Wakati huo huo leo hii maelfu ya watu wanaopinga vitendo vya kigaidi wamekusanyika katika maandamano makubwa kwenye mji mkuu wa Ufaransa, Paris, maandamano ambayo yamehudhuriwa pia na viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbalimbali duniani.

Maandamano hayo yamefanyika baada ya siku kadhaa za mashambulizi ya watu wenye silaha mjini Paris ambayo yamepelekea watu 17 kuuawa wakiwemo watu watatu waliofanya mashambulizi hayo.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema, leo Paris imekuwa ni mji mkuu wa dunia, kutokana na watu kutoka pembe mbalimbali duniani kukusanyika mjini humo kupinga vitendo vya kigaidi.../mh

2700807

captcha