IQNA

Iran yasikitishwa na mauaji ya Waislamu nchini Nigeria

14:48 - December 14, 2015
Habari ID: 3463095
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeitaka serikali ya Nigeria kuwaheshimu viongozi wa kidini na maeneo matakatifu, siku moja baada ya jeshi la nchi hiyo kumkamata kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky, baada ya kutekeleza hujuma nyumbani kwake kaskazini mwa nchi hiyo.

Hossein Jaberi-Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema: “Nigeria kwa sasa inakabiliwa na matatizo mengi yanayotokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri na lenye misimamo iliyofurutu ada la Boko Haram na hivyo katika hali hiyo tunahisi unahitajika umoja wa kitaifa na mshikamano.” Jaberi-Ansari ameeleza kusikitishwa kwake na umwagaji damu uliosababishwa na vyombo vya usalama viliposhambulia Waislamu siku ya Jumapili na Jumamosi
Baadhi ya duru zinasema hadi sasa jeshi la Nigeria limeua zaidi ya Waislamu 100 wa madhehebu ya Shia tangu kuanza kwa ghasia katika ukumbi wa kidini wa Husseiniya Baqiyatullah katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema Naibu wa Sheik Zakzaky, Sheikh Mohammad Turi ameuawa kwa kupigwa risasi katika machafuko hayo.
Watetezi wa haki za binadamu wameilaumu vikali serikali ya Nigeria kwa kukiuka haki za kidini na kijamii kwa kushambulia mijumuiko ya amani ya Mashia. Mwezi Julai mwaka jana karibu Waislamu 24 wa madhehebu ya Shia waliuawa baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds.

3462943

Kishikizo: iran nigeria jaberi mashia
captcha