IQNA

Waislamu wanaodhulumiwa

Ayatullah Sistani alaani hujuma za kigaidi dhidi ya Mashia nchini Pakistan

15:53 - November 23, 2024
Habari ID: 3479796
IQNA - Kiongozi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq amelaani vikali shambulio la kigaidi nchini Pakistan lililogharimu maisha ya zaidi ya Waislamu 40 wa Kishia.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, Ofisi ya Ayatullah Seyed Ali Sistani, imelaani shambulio hilo la kigaidi na kusema ni "uhalifu wa kutisha," ikibainisha kuwa hatua hizo zinalenga "kudhoofisha umoja wa Waislamu."
"Tunatoa wito kwa serikali tukufu ya Pakistan kuchukua hatua zinazohitajika ili kuwalinda raia wake dhidi ya ukandamizaji na uhalifu wa makundi ya kigaidi," alisema.
Ni muhimu kuhakikisha kwamba waumini wasio na hatia hawashambuliwi na makundi yenye itikadi kali na yasiyo na huruma, aliongeza.
Takriban Waislamu 42 wa madhehebu ya Shia waliuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika shambulizi dhidi ya msafara katika wilaya ya Kurram nchini Pakistan, katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa. Shambulizi hilo la kuvizia lilitokea wakati msafara huo ukisafiri kutoka Parachinar hadi Peshawar, siku chache baada ya kufunguliwa tena kwa barabara kuu kuu kufuatia hujuma za magaidi wakufurishaji.

Vikosi vya usalama vya Pakistan kwa sasa vinafanya oparesheni za kijasusi katika maeneo mbalimbali yasiyo na usalama nchini humo kuwasaka magaidi hao.

3490787

Habari zinazohusiana
Kishikizo: pakistan mashia
captcha