
Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Ansarullah nchini Yemen amesema
kuwa, madai yanayotolewa na utawala wa Aal-Saud kwamba harakati hiyo na
jeshi la Yemen imeshambulia msikiti wa Makkah, ni njama za kuamsha hisia
za Waislamu duniani kwa lengo la kuomba msaada toka kwao baada ya
kushindwa vita.
Mohammad Abdus Salam, amewataka Waislamu duniani kupuuza madai hayo ya
uongo yanayoenezwa na muungano vamizi wa Saudia sanjari na kuyataja kuwa
yasiyo na maana. Abdus Salam amesema kuwa, Wayemen hawahitaji hisia za
kidini wala za Kiarabu na kwamba jeshi la taifa hilo licha ya
mashambulizi ya kila upande yanayotekelezwa na Saudia na waitifaki wake
ikiwemo Marekani na utawala haramu wa Israel na kadhalika hasara kubwa
iliyolenga miundombinu, hawajawahi kushambulia hata taasisi moja ya
Saudia, achilia mbali maeneo matakatifu ya kidini kama vile Nyumba ya
Mwenyezi Mungu al-Kaabah.
Itafaa kuashiria kuwa, Alkhamis iliyopita, jeshi la Yemen liliushambulia
kwa kombora aina ya Burkan 1 uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mfalme
Abdulaziz mjini Jeddah, magharibi mwa Saudia na kusababisha hasara
kubwa. Duru za ndani nchini Saudia zinaarifu kwamba, kufuatia shambulio
hilo, utawala wa Aal-Saud ulipatwa na wasi wasi mkubwa na hivyo asubuhi
ya Ijumaa ukadai kuwa, kombora moja lilirushwa na jeshi la Yemen kutoka
mji wa kaskazini mwa Saada kuelekea mji mtukufu wa Makkah, huku jeshi la
Yemen likishangazwa na madai hayo yenye lengo la kuibua hisia za
Waislamu duniani.
Kufuatia madai hayo, baadhi ya duru nchini Saudia zilifichua kuwepo
njama za watawala wa Aal-Saud za kutekeleza shambulizi dhidi ya maeneo
matakatifu ya kidini na kisha kuitwisha lawama harakati hiyo ya Kiislamu
ya Answarullah nchini Yemen, ambayo hadi sasa imeweza kufelisha malengo
machafu ya Saudia na waitifaki wake ndani ya Yemen.
3541305