IQNA

Mwanae Hayati Muhammad Ali akamatwa Marekani kwa kuwa na jina la Kiislamu

11:17 - February 26, 2017
Habari ID: 3470868
IQNA-Mwanae bingwa wa masumbwi duniani marehemu Muhammad Ali, ametiwa mbaroni katika uwanja wa ndege wa jimbo la Florida nchini Marekani kwa sababu tu an jina la Kiislamu.
Muhammad Ali Junior, mmoja wa watoto wa marehemu Muhammad Ali, alitiwa mbaroni katika uwanja wa ndege wa jimbo la Florida wakati alipokuwa akirejea kutoka nchini Jamaica kuingia Marekani. Habari zaidi zinasema kuwa, baada ya kutiwa mbaroni mwana huyo wa Muhammad Ali alihojiwa kwa masaa mawili. 
Muhammad Ali Junior alizaliwa katika mji wa Philadelphia katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani huku akiwa na pasi ya kusafiria ya nchi hiyo. Junior anaishi nchini Jamaica pamoja na mama yake, Khalilah Camacho Ali. Wakili wa mwana huyo wa Muhammad Ali, kwa jina la Chris Manshny amesema kuwa kijana huyo wa mwanamasumbwi mashuhuri duniani na mama yake walitiwa mbaroni katika uwanja huo wa ndege wa Florida mwezi huu kutokana na kuwa na majina ya Kiarabu.

Kwa mujibu wa wakili huyo, Bi, Khalilah Camacho Ali na mwanaye waliachiliwa, mara baada ya kuonyesha picha inayomuonyesha yeye akiwa na marehemu mume wake huku wakiwa tayari wamehojiwa kwa muda usiopungua masaa mawili. 
Tangu Rais Donald Trump wa Marekani aliposaini marufuku ya kuzuiwa raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini  humo, Waislamu wamekuwa wakikumbwa na madhila mbalimbali ndani ya taifa hilo linalojinadi kuwa mtetezi wa haki za binaadamu duniani. Hii ni katika hali ambayo mahakama kadhaa za nchi hiyo zimetaka kutupiliwa mbali marufuku hiyo ya Rais Trump.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa, asilimia 60 ya Waislamu wa Marekani wanashtakia na kulalamikia ubaguzi, taasubi dhidi ya Uislamu pamoja na propaganda na hisia za chuki dhidi ya dini ya Kiislamu. Vyombo vya habari vya Marekani navyo vimekuwa vikieneza propaganda na hisia za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na kufanya njama za kuonyesha kuwa dini hiyo tukufu haina tofauti na misimamo ya kuchupa mipaka. Trump ambaye katika kampeni zake za uchaguzi alionesha wazi misimamo yake ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, anaonekana kushikilia misimamo yake hiyo hadi sasa ikiwa ni majuma kadhaa tu kabla ya kuapishwa na kuanza rasmi kipindi chake cha uongozi.

captcha