IQNA

Kumbukumbu ya jinai ya kuteketezwa moto Msikiti wa Al Aqsa

0:23 - August 22, 2017
Habari ID: 3471136
TEHRAN (IQNA)- Agosti 21 miaka 48 iliyopita, yaani mwaka 1969 Miladia, Msikiti wa al-Aqsa Kibla cha Kwanza cha Waislamu ulihujumiwa na kuteketezwa moto na Wazayuni kwa himaya ya utawala haramu wa Israel.

Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria katika mji wa al Quds (Jerusalem) liliharibika vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mhalifu huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).

Aidha Siku ya Kimataifa ya Msikiti huadhimishwa kila mwaka nchini Iran na katika baadhi ya nchi duniani ili kukumbuka tukio la kuchomwa moto Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Mwaka 1969 Mzayuni Michael Dennis Rohan aliuteketeza kwa moto msikiti huo. Wakati huo maafisa wa Israel walitangaza kuwa mtu huyo aliyekuwa na uraia wa Australia, ni Mkisto mwendawazimu, lakini baadaye ilibainika kuwa Dennis Rohan ni Myahudi mwenye misimamo ya kuchupa mipaka na alichoma moto kibla hicho cha kwanza cha Waislamu kwa makusudi. Mbali na hayo ushahidi ulionesha kuwa Wazayuni wengine wenye misimamo mikali walimsaidia Michael Dennis Rohan katika harakati zake za kuchoma msikiti huo.

Quds na maeneo yake matakatifu yamekuwa yakishambuliwa na kuvunjiwa heshima tangu Wazayuni walipovamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Katika kipindi chote cha miongo kadhaa iliyopita utawala wa kikatili wa Israel si tu kwamba hauwaonei huruma watoto wadogo na wanawake na umekuwa ukifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, bali pia umekuwa ukivunja na kuhujumu misikiti na makanisa ya eneo hilo. Pamoja na hayo Msikiti wa al Aqsa ndio unaoshambuliwa na kuvunjiwa heshima zaidi kati ya maeneo yote matakatifu ya Palestina na hilo linafanyika ili kuuharibu kabisa msikiti huo na hatimaye kufuta kabisa utambulisho wa kihistoria wa Palestina. Utawala bandia wa Israel daima umekuwa ukilipa kipaumbele suala la kufuta utambulisho wa Kiislamu wa Quds tukufu na kuharibu maeneo matakatifu na ya kihistoria ya mji huo.

Israel hususan katika miongo miwili iliyopita ya mazungumzo na Wapalestina, imejenga majumba ya kamari, mahoteli, vituo vya anasa na maeneo ya ufuska kandokando ya Msikiti wa al Aqsa kwa shabaha ya kuuzingira msikiti huo. Vilevile utawala huo ghasibu unachimba njia za chini ya msikiti huo kwa lengo la kuuharibu.

3632711

captcha