IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuhitimishwa satwa ya ISIS ni pigo kwa Marekani na vibaraka wake Mashariki ya Kati

20:37 - November 22, 2017
Habari ID: 3471274
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuhitimishwa satwa ya mti khabithi wa kundi la kigaidi la ISIS ni pigo kwa serikali za huko nyuma na za sasa za Marekani pamoja na tawala vibaraka na tegemezi kwa Washington katika Mashariki ya Kati ambazo zililianzisha kundi hili na kuliunga mkono kwa hali na mali ili zitanue satwa zao katika eneo hili na hivyo kuufanya utawala ghasibu wa Israel uwe na udhibiti wa eneo hili.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo Jumanne katika jibu lake kwa barua ya Meja Jenerali Qassem Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza : "Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mkubwa ambaye amezipa baraka juhudi zako za kujitolea kijihadi pamoja na wenzako katika nyuga mbalimbali na hivyo kupelekea kung'olewa kwa mikono yenu nyinyi waja wema huko Syria na Iraq mizizi ya mti khabithi wa ISIS ambao mche wake ulipandwa na mataghuti wa dunia."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hili sio pigo kwa kundi ovu na dhalimu la ISIS pekee, bali hatua hiyo ya kung'olewa mizizi ya ISIS imetoa pigo kubwa pia kwa siasa za kikhabithi za kuanzisha vita vya ndani katika Mashariki ya Kati na kuutokomeza muqawama ulio dhidi ya Israel sambamba na kuyadhoofisha madola na tawala huru kupitia viongozi waovu wa kundi hilo lililopotoka.

Katika sehemu nyingine ya jibu lake kwa barua hiyo, Ayatullah Khamenei amemhutubu Meja Jenerali Qassem Suleimani kwa kumwambia: "Kwa hatua yako na wenzako ya kulisambaratisha donda hili angamizi la saratani, mumezihudumia pakubwa si nchi za Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa Kiislamu pekee, bali mataifa yote na jamii nzima ya mwanadamu.

Kadhalika Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa kheri na pongezi kwa ushindi huo na kubainisha kwamba, haipasi kughafilika na hila na ghiliba za adui."

Mapema jana Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, alimtumia ujumbe Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akitangaza kuangamizwa satwa khabithi ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Kwa mujibu wa tovuti ya Sepahnews, Meja Jenerali Qassem Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumanne asubuhi amemtumia ujumbe Ayatullah Khamenei na kutangaza kuwa: "Mimi kama mtumishi na askari mwenye kutekeleza wadhifa kwa niaba yako katika medani hii, ninatangaza hapa kuwa, kufuatia kukombolewa mji wa Al Bukamal, ngome ya mwisho ya ISIS na bendera ya kundi hili la Kimarekani-Kizayuni imeshushwa na mahala pake kupeperushwa bendera ya Syria na kwa msingi huo satwa khabaithi na iliyolaaniwa ya ISIS imefika ukingoni."

3464488/

captcha