IQNA

Rais Hassan Rouhani wa Iran
12:12 - May 19, 2018
News ID: 3471521
TEHRAN (IQNA)-Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa wito kwa nchi za Kiislamu na mataifa mengine duniani kukata uhusiano wao kikamilifu na utawala haramu wa Israel na kuangalia upya uhusiano na Marekani kama njia ya kujibu sera hasimu za tawala hizo mbili dhidi ya watu wa Palestina.

Akizungumza katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Istanbul Uturuki Ijumaa, Rais Rouhani amelaani vikali mauaji yaliyofanywa hivi karibuni na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Aidha amelaani uamuzi wa rais Donald Trump wa Marekani wa kuhamisha ubalozi wa nchi hiyo kutoka Tel Aviv hadi mji wa Quds (Jerusalem) huku akiwasilisha mapendekezo kadhaa kuhuhusu namna ya kuhitimisha sera hizo hasimu.

Rais Rouhani amesema: "Ili kuwasaidia Wapalestina na kukabiliana na uamuzi haribifu wa Trump, tunatoa wito kwa nchi za Kiislamu na mataifa yote yanayopenda uhuru duniani kuangalia upya uhusiano wao wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara na Marekani sambamba na kukata uhusiano wote na utawala wa Kizayuni (wa Israel) na kususia bidhaa na mashirika ya Kizayuni."

Umoja wa Mataifa uchukue hatua

Rais Rouhani aidha ametaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likutane kujadili hatua iliyo kinyume cha sheria ya Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds na pia jinai za hivi karibuni za utawala haramu wa Israel huko Ghaza. Rais wa Iran pia ametaka OIC ianzishe mkakati wa kuwafikishia misaada ya kibinadamu Wapalestina na pia kutambuliwa Siku ya Kimataifa ya Quds katika kalenda ya nchi zote za Kiislamu. Rais wa Iran pia ametaka OIC iushinikize utawala haramu wa Israel uangamize silaha zake hatari za nyuklia.

Rais Rouhani amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitekeleza jinai na ukatili dhidi ya Wapalestina kwa miaka sabini sasa na kwamba utawala huo umekiuka sheria na kanunui zote za kimataifa. Rais Rouhani amesema utawala wa Kizayuni umewanyima Wapalestina haki zao za kimsingi na umekuwa ukiwasilisha sera zake za ubaguzi wa rangi na misimamo mikali ya kidini kuwa eti ni demokrasia. Amesema ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zimekuwa zikitetea jinai hizo za Israel. Rais Rouhani ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuungana na kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina.

Erdogan: Israel iwajibishwe

Akiuhutubia mkutano huo, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, ambaye ni mwenyekiti wa kiduru wa OIC, ameahidi kufuatia jinai za Israel huko Ghaza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Amesema utawala haramu wa Israel unapaswa kuwajibishwa kutokana na jinai zake dhidi ya Wapalestina. Rais wa Uturuki pia ameikosoa vikali Marekani kwa kuzuia hatua zote zinazochukuliwa kuiadhibi Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Saudia, Misri zasusia mkutano wa Palestina

Baada ya mkutano huo wa OIC mjini Istanbul, viongozi walioshiriki walitoa taarifa ya mwisho ambayo ilitaka kuundwe kamati ya kuchunguza jinai za Israel huko Ghaza sambamba na kuanzishwa kikosi cha kimataifa cha kuwalinda Wapalestina. Aidha nchi 57 za OIC zimetoa wito kwa mataifa yote duniani kujadili jinai za Israel katika Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa nchi muhimu za Kiislamu katika eneo lakini watawala wa Saudi Arabia na Misri walisusia mkutano huo muhimu.

3715469

Name:
Email:
* Comment: