IQNA

22:08 - May 10, 2019
News ID: 3471950
TEHRAN (IQNA)- Wananchi wa Iran ya Kiislamu wameandamana nchi nzima baada ya Sala ya Ijumaa kuunga mkono hatua zilizochukuliwa na serikali ya Iran kusimamisha utekelezaji wa baadhi ya ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).

Taarifa zinasema kuwa wananchi wa Iran katika kona zote za nchi wamefanya maandamano makubwa baada ya Sala ya Ijumaa ya leo huku wakipiga nara za "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel"  na ‘Ushindi kwa Uislamu” ambapo wametangaza kuunga mkono kuchukuliwa hatua madhubuti za kukabiliana na tabia mbaya za Marekani na Ulaya za kutotekeleza ahadi zao katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Mwishoni mwa maandamano yao, wananchi wa Iran wametoa taarifa na kuwaonya viongozi wa Marekani wakisema, hatua yoyote ya kutoa vitisho kwa Iran itakumbwa na majibu makali ya wananchi wa taifa hili kubwa la Kiislamu.

Wananchi wa Iran wametangaza pia kuwa hawana imani hata kidogo na madola ajinabi na kamwe hawatosalimu amri mbele ya matakwa ya kibeberu ya waistikbari wa dunia. Aidha wameitaka serikali ya Iran kuchukua hatua kali zaidi za kukabiliana na taiba ya Marekani na Ulaya ya kukwepa kutekeleza ahadi zao za JCPOA.

Juzi Jumatano tarehe 8 Mei 2019 Iran ilitangaza kusimamisha baadhi ya ahadi zake ilizozitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuzipa pande zilizobakia kwenye mapatano hayo, muda wa siku 60 kuhakikisha kuwa zinatekeleza ipasavyo ahadi zao.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema siku ya Jumatano kwamba Tehran itaongeza akiba ya urani yake iliyorutubishwa pamoja na maji mazito ya nyuklia na kama katika kipindi cha siku 60 nchi za Ulaya zitashindwa kuchukua hatua za kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, basi Tehran itaanza kutengeneza kinu cha nyuklia.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran ameashiria kusitishwa baadhi ya hatua za Iran katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jamii ya kimataifa na madola ya Ulaya yaliyoko katika makubaliano ya JCPOA yanakabiliwa na mtihani mgumu.

Hujjatul Islam Muhammad Javad Haj Ali Akbari amesema hayo leo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya kimaanawi na kisiasa ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran ambapo amesisitiza kwamba, umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran ambao ni wa kupigiwa mfano unawashinda maadui.

Ameeleza kuwa, hasira za madola ya Ulaya baada ya kusitishwa baadhi ya hatua za Iran katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), ni ishara ya wazi kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya harakati katika njia sahihi kwa ya kufikia malengo yake.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya wiki hii hapa mjini Tehran amesisitiza kuwa, kusitishwa baadhi ya hatua za Iran katika makubaliano ya JCPOA ni hatua ya awali na utangulizi tu ambapo kama madola ya Ulaya hayatatekeleza ahadi zake katika makubaliano hayo, Iran itachukua hatua nyingine baada ya kumalizika muhula huo wa siku 60.

/3810315

Name:
Email:
* Comment: