IQNA

11:29 - March 16, 2020
News ID: 3472570
TEHRAN (IQNA)- Serikali ya Kuwait imefunga kwa muda misikiti nchini na kubadilisha adhana kufuatia hofu ya kuenea ugonjwa wa COVID-19 maarufu kama corona.

Siku ya Ijumaa , Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu Kuwait ilitangaza kuwa,  adhana sasa zitaongezwa maneno yafuatayo, ‘Swalini katika Majumba Yenu” -الصلاة في بيوتكم- ili kuwahimiza waumini wasiende misikitini bali waswali ndani ya nyumba zao ili kuzuia kuenea COVID-19, ugonjwa ambao huenea haraka katika maeneo yenye mijumuiko.

Wizara ya  Wakfu na Masuala ya Kidini Kuwait imesema hatua hiyo ni ya muda.  Aidha wakuu wa Kuwait wametangaza likizo ya kitaifa kuanzia Machi 12 hadi 26 lakini wanaotoa huduma za dharura wataendelea kufanya kazi.

Halikadhalika migahawa imefungwa na pia maeneo ya kibiashara nayo pia yamefungwa kwa muda. Kuanzia Ijumaa iliyopita safari zote za ndege za za abiria katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mji wa Kuwait zimesitishwa. Hadi kufikia Ijumaa, kulikuwa na kesi 100 za kirusi cha corona nchini Kuwait lakini hakuna kifo chochote kilichoripotiwa. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, hadi kufikia 15 Machi, watu waliokuwa wameambukizwa COVID-19 kote duniani wamepindukia 152,428 huku waliofariki wakiwa ni zaidi ya 5,720 katika nchi 141 kote duniani.

3885322

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: