IQNA

8:30 - March 19, 2020
News ID: 3472580
TEHRAN (IQNA) – Misikiti kadhaa muhimu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi imefungwa kutokana na hofu ya kuenea ugonjwa wa COVID-19 maarufu kama kirusi cha corona.

Msikiti wa kwanza kutangaza kufungwa kwa muda ni Msikiti wa Jamia kati kati ya jiji la Nairobi. Katika taarifa, kamati ya msikiti huo imesema: "Baada ya mashauriano na Baraza la Maulamaa wa Msikiti wa Jamia na pia kufuatia mashauriano na Jumuiya ya Waislamu Wanaofanya Kazi za Kitaalamu katika Sekta ya Tiba (KAMMP), Kamati ya Msikiti wa Jamia imeamua kuwa, kuanzia Jumatano Machi 18, sala zote za jamaa zitasitishwa kwa muda katika Msikiti wa Jamia."

Aidha Msitiki wa Al Huda katika mtaa wa South B Nairobi nao pia umetoa taarifa na kusema kufuatia agizo la serikali la kupiga marufuku mijumuiko ili kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19, kamati ya msikiti imeamua kuwa sala zote zitasitishwa kwa muda kuanzia Machi 19. Halikadhalika kamati ya Msikiti wa Parklands mjini Nairobi imesema msikiti huo utafungwa kwa muda ili kuzuia maambukizi ya kirusi cha corona. Vile vile msikiti wa mtaa wa Hurlingham, Masjid ur Rahma nao pia umetangaza kufunga milango yake kwa muda.

Nayo kamati ya Masjid Imtiaz imetangaza kuwa msikiti huo ambao pia uko kati kati ya jiji la Nairobi nao pia umefungwa kwa muda. Katika taarifa, mwenyekiti wa kamati ya msikiti huo  Rafiq Miyanji amesema baada ya mashauriano na wanazuoni nwa wataalamu wa tiba, wameauamu kufunga msikiti ili kuzuia kuenea ugonjwa wa corona. Amesema adhana itaendelea kama kawaida katika msikiti huo lakini itabadilishwa, kwa mujibu wa Sunna, ambapo ibara ifuatayo itatamkwa na muadhini: "Swalini katika Majumba Yenu".

Hadi sasa watu saba wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19 nchini Kenya na hivyo kuna hofu kuwa homa hiyo hatari itaenea kwa kasi iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: