IQNA

Raia wa Marekani afadhilisha kubakia Iran katika kipindi hiki cha janga la corona

11:56 - March 18, 2020
Habari ID: 3472578
TEHRAN (IQNA) – Mwandishi habari Mmarekani anayeishi nchini Iran amesema anafadhilisha kubakia Iran wakati huu wa kuenea maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 maarufu kama kirusi cha corona kutokana na ukarimu na mshikamano wa Wairani katika kukabiliana na uvonjwa huu.

Bi. Jennifer Green, Mmarekani ambaye tokea ugonjwa wa COVID-19 utangazwe kugundulika amekuwa nchini Iran ameandika makala katika tovuti ya elemental.medium.com na kubainisha kuhusu uzoefu wake katika kipindi hiki.

Anasema aliwasili Iran Aprili mwaka 2019 na alitaraji kuwa wakati huu angekuwa amesharejea nyumbani nchini Marekani, lakini aliahirisha safari hiyo mara kadhaa na sasa baada ya mashirika mengi ya ndege kufuta safari zao, hawakuweza kusafiri. Bi. Green anasema awali waliingiwa na wasiwasi mkubwa baada ya kirusi cha corona kuripotiwa Iran lakini sasa imebainikia kuwa maeneo yote duniani si salama kutokana na kuenea ugonjwa huo kila mahala. Anaongeza kuwa, baada ya kusoma kwenye vyombo vya habari vya Magharibi na kuona clipu za video kuhusu namna Wamagharibi walivyofurika katika masupamaketi kwa fujo kununua  dawa au sabuni za kuosha mikono na karatasi za chooni na maski, alifikia natija kuwa ni bora kubakia Iran katika kipindi hiki cha janga la corona.

Bi. Green anasema pamoja na kuwa masoko ya matunda, supamaketi, na maduka mengine yamekuwa yakijaa wateja mjini Tehran katika kipindi hiki cha corona, lakini wote wanasimama katika foleini kwa nidhamu wakisubiri zamu yao. "Sijashuhudia watu wakisukumana na kupokonyana bidhaa. Bidhaa zimejaa na hakuna upungufu wowote nilioshuhudia na ninapata kila kitu ninachohitajia." Anasema awali kulikuwa na uhaba wa baadhi ya bidhaa kama vile maski na katika baadhi ya maeneo ziliuzwa kwa bei ya juu  na baadhi ya watu wenye kujitakia faida. Aidha ansema pia awali kulikuwa na uhaba wa malimau, tangawizi na kitunguu saumu lakini sasa hali imerejea kama ya kawaida.

Anaongeza kuwa hakuna uhaba wa makaratasi ya chooni nchini Iran kwa sababu Wairani kwa kawaida hutumia maji kujitwahirisha.

Mmarekani huyu ambaye yuko safarini nchini Iran anasema mwaka mpya wa Kiirani au Nairuzi, ambao huanza Machi 21, utakuwa tafauti mwaka huu kwani serikali imezuia safari baina ya miji ili kuzuia kuenea kirusi cha corona.

Bi. Greens anasema pamoja na kuwa Iran iko katika mashinikizo makali ya Marekani lakini ameshuhudia ukarimu wa aina yake katika nchi hii ya Kiislamu. Kati ya vitendo vya ukarimu  alivyoshuhudia wakati huu wa janga la corona ni watu wanaojitolea kutumia kemikali maalumu kusafisha mashine za ATM za benki, wananchi wanajitolea kusambaza glavu kwa watu wasiojiweza ambao hukusanya takataka na kuzuiuza na wakulima katika eneo moja la Khorassan Razavi ambao wamejitolea kusambaza glavu, maski, pamoja na kemikali za kuua vijidudi. Aidha Bi. Green anasema kuna baadhi ya wenye nyumba ambao wamefuta kodi za nyumba kwa muda wa miezi miwili na wataalamu wa mikrobiolojia waliojitolea kufanya kazi za vipimo vya corona. Aidha amesema serikali imewapatia wananchi intaneti bila malipo kwa muda wa wiki mbili ili wabakie nyumbani. Anaongeza kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaowasiadia wafanyakazi wenzao na majirani kwa njia mbali mbali kukabiliana na corona kama vile kuwapa dawa au sabuni kemikali malaumu za kuua virusi.

"Wairani wanaamini kuwa, iwapo unataka kubakia salama na usiambukizwe kirusi cha corona, basi unapaswa kuwalinda walio karibu nawe. Utawezaje kuwa salama iwapo jirani yako ataambukizwa," ameandika Bi. Green.

Kwa ujumla anasema pamoja na kuwa Iran imeathiriwa vibaya na ugonjwa wa COVID-19, lakini nchi hii ingali inashuhudia ukarimu mkubwa wa kibinadamu.

Mmarekani huyo anamaliza kwa kuandika kuwa kirusi cha corona hakijuia tajiri wala masikini, au rangi, dini na jiografia na kwamba kama wanavyosema Wairani, kusaidiana pamoja kutatuwezesha kuvuka kipindi hiki kigumu.

3886089

captcha